MBUNGE wa jimbo la Vunjo, Dkt Charles Kimei ametoa vifaa vya michezo kwa timu 16 vyenye thamani ya Tsh mil 8.5 kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya kugombea Kombe la Vunjo ‘Vunjo Cup’ litakalofanyika Desemba 22 mwaka huu.......Na Gift Mongi Moshi
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo, kwenye ofisi yake ya jimbo, Dkt Kimei alisema ametoa vifaa hivyo kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuendeleza michezo kwa vijana.
Vifaa alivyokabidhi mbunge huyo ambaye kabla ya kuingia kwenye siasa, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB nchini, ni pamoja na seti moja ya jezi kwa timu hizo, mipira, firimbi, saa na kiasi cha fedha taslimu cha sh 100,000 kwa kila timu kwa ajili ya maandalizi.
Alisema anatambua umuhimu wa vijana katika ushiriki wa michezo ambapo pamoja na kujenga afya yao ya mwili lakini pia unaibua vipaji vitakavyowasaidia kuweza kusajiliwa na timu kubwa na ndiyo maana ameamua kuanzisha mashindano hayo.
“Vijana natambua umuhimu wenu katika jimbo letu, nimeanzisha mashindano haya ya ‘Vunjo Cup’ ili kuwaweka karibu lakini pia kuibua vipaji vyao maana mpira ni ajira na kupitia mashindano haya mnaweza kusajili na timu kubwa,” alisema Dkt Kimei na kuitaka kila timu ikajiandae vizuri ili kupambania zawadi.
Alitangaza kwamba mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atazawadiwa zawadi ya shilingi milioni mbili na nusu (Tsh mil 2.5), mshindi wa pili atapata shilingi milioni moja na nusu (Tsh mil 1.5) huku mshindi wa tatu atajiondokea na shilingi milioni moja (Tsh mil 1).
0 Comments