NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Bodi ya mikopo wanafunzi wa Elimu ya juu (HESLB) imekusanya zaidi ya billion 182 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kutokana na hali ya urejesha kuwa nzuri tofauti na awali ambapo wanatarajia kukusanya billion 185 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Hayo yameelezwa na Afisa mawasiliano mkuu wa bodi hiyo Veneranda Malima wakati akiongea na waandishi wa habari katika maonesho yaliyoenda sambamba kongamano la mwaka la 31 la wahandisi lilifanyika mkoani Arusha ambapo alisema kuwa miaka ya nyuma walivyoanza kukusanya makusanyo yalikuwa kidogo lakini kwanzia mwaka 2016/2017 yakianza kuongezeka.
“Bodi ilianzishwa mwaka 2005 lakini tulianza kukusanya madeni mwaka 2007 na wakati huo makusanyo yalikuwa kidogo kidogo lakini kwanzia 2016/2017 tumeanza kukusanya kwa kiasi kikubwa na mwaka ulioisha 2020/2021 tmekusanya shilingi billion 182 na tunategemea kwa mwaka huu ulioanza wa 2021/2022 tutakusanya bilioni 185,” Alisema Veneranda.
Alisema kuwa kwa mwelekeo huo wanaona urejeshaji unaenda vizuri na wameshiriki katika maonesho hayo kwasababu wahandisi wengi ni wanufaika wa mikopo hiyo na wanapita katika banda lao kupata taarifa za madeni yao na wanaweza kuangalia ni kiasi gani wanadaiwa na walio tayari kwaajili ya kulipa wanaweza kulipa lakini pia kujua muendelezo wao wa urejeshaji.
Alifafanua kuwa walio katika sekta isiyo rasmi kiwango chao cha kurejesha ni shilingi laki moja kwa mwezi na halazimiki kutoa zote kwa pamoja bali anaweza akatoa kidogo kidogo ndani ya mwezi hadi ikatimia na wale ambao wana uwezo mkubwa wanawakaribisha waweze kulipa madeni yao yote.
“Tuna kampeni ambayo tunaita kampeni ya kusifurisha ambayo madeni mengi kwa sasa yanaweza yakalipwa kwa mkupuo kwasababu mengi hayana tozo ya kulinda thamani wala hayana tozo ya adhabu ile ya asilimia kumi kwahiyo tunawakaribisha wote waweze kurejesha kama ambavyo wao walionufaika basi na wafunzi wengine wa vyou vikuu wanaoanza waweze kunufaika,” Alisema.
0 Comments