Header Ads Widget

CHAPUO LA MASOMO YA ZIADA III

 




Nina ndugu yangu mmoja anaitwa Philbert Masele, huyu ni ndugu yangu tangu tukiwa watoto yeye nadhani Msukuma/Mnyamwezi. Novemba 29, 2021 aliyaandika maneno katika kurasa yake ya facebook.....NA ADELADIUS MAKWEGA_MBAGALA.


“In business, what you don’t get done today can be done tomorrow. But with family, what does not get done today is gone forever.”


“Katika biashara jambo ambalo umeshindwa kulifanya leo, utalifanya kesho. Lakini katika masuala ya familia, lile uliloshindwa kulifanya leo, ndiyo kwaheri.”


Huyu ni Mtanzania mwezetu nadhani yupo ng’ambo hivi sasa kabila lake kama nilivyosema ni Msukuma/ Mnyamwezi wa Darisalaam siyo wa Mwanza/Tabora/Shinyanga maana namfahamu baba na mama yake ambao leo hii(wazazi wake) ni marehemu. Haya maneno aliyoyaandika ni mazito sana. Maneno haya aliyaambatanisha na picha anayoonekana yeye mwenyewe, mkewe na watoto wake wakiwa nyuma katika chombo cha usafiri.


Maneno haya nayahusianisha na umuhimu wa elimu kwa watoto katika familia. Kwani familia ni Baba, mama, watoto na hata familia zile ya wajomba, shangazi, baba na watoto pekee yake na mama na watoto peke yake. Familia ina wajibu wa kuwapatia watoto mavazi, chakula na hata elimu kwa ustawi wa watoto hao na kwa maslahi yao ya sasa na ya baadae.


Kwa maelezo ya ndugu Philbert usipolitilia maanani suala la elimu ya watoto kwa sasa kama ninavyotafsiri mimi jambo hilo litakuwa limekwenda na maji, kwa ndugu zangu wahehe jambo hilo litakuwa ni TWIWONAGA yaani kwaheri ya BURIANI.


Hivi karibuni zimetolewa kauli mbili za mawaziri wanaosimamia elimu nchini yaani WAZIRI WA ELIMU na WA TAMISEMI juu ya msitisho wa masomo ya ziada.


“Kipindi cha likizo ni kipindi cha kupumzika pengine mzazi anataka mtoto aende naye likizo, lakini pia masomo haya ya ziada yamekuwa kichochoro cha kutoza gharama na yana gharama kubwa kuanzia 5000-250,000/. Kwa hiyo ninawasisitiza kuwa maafisa elimu kuzingatia waraka wa elimu nambari tatu wa mwaka 2016.” Huyu ni waziri wa Elimu.


“Ni marufuku kwa watoto wa shule za msingi na sekondari za serikali kusoma masomo ya ziada, nitawasiliana na waziri wa Elimu katika hili na hapa ninaye Kamishina wa Elimu.” Huyu ni Waziri wa TAMISEMI.


Swali ni jee huo waraka wa Elimu unasema nini? Katika Barua hii (Waraka huu) imegawanya majukumu kwa Wizara ya Elimu Sayansi Tekinolojia(4), TAMISEMI(7), Sekretarieti za Mikoa(5), Wakuu wa Wilaya(4), Wakurugenzi Watendaji (13), Wakuu wa shule(10), Bodi/Kamati za shule (4), Walimu(5), Wanafunzi(4) , Wazazi/ walezi(6) na Viongozi wa jamii (4). Kwa mujibu wa barua hii kila mmoja amekabidhiiwa orodha ya majukumu ambapo mimi nimeyaweka katika mabano kwa namba hapo juu.


Kwa leo nitazame tu majukumu ya Bodi/Kamati za shule na Wazazi / Walezi wenye watoto katika shule za serikali.


Kamati na Bodi za shule za serikali zitaendelea kuwa kiungo muhimu cha wazazi na walezi na shule. Aidha zihakikishe kuwa zinasimamia vema uendeshaji wa shule. 


Aliyetayarisha waraka huu alikuwa ni mtu mwenye mwelevu akayasema mambo mane. La kwanza, la pili na la tatu hapa ninalinukuu:


“Kamati /Bodi za shule zishirikiane na jamii katika maazimio ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na mendeleo ya shule kwa ujumla kama vile ulinzi wa shule na upatikanaji wa walimu wa muda(temporay / part time teachers) kwa masomo ya Sayansi, Hisabati na ufundi. Maazimio yanayohusu uchangishaji wa hiari, yawasilishwe kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa lengo la kupata kibali.” 3.7. III ya Waraka huu.


Kwa maelezo haya waraka unatambua kuwa walimu wa sayansi hawapo wa kutosha na hawatopatikana bure lazima wazazi watachangishwa na kibali wataomba kwa mkurugenzi mtendaji.Kwa ukweli wa Mungu huyu Mkurugenzi Mtendaji ubavu wa kuwanyima kibali hana. Ubavu huo anaweza kuwa nao kama angewezesha kupatikana walimu hao. Nakukumbusha kuwa hapo pia wametaja walinzi wa shule hizo. Kuchangisha hakukwepeki kabisa.


Waraka huu ukaenda mbali zaidi katika 3.7. IV inasema 


“Bodi/Kamati za shule zitahakikisha zinashirikiana na Wazazi/ jamii kuweka utaratibu wa chakula mchana shuleni na huduma za Hosteli katika shule za kutwa kulingana na mazingira yao na kutuma mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Halimashauri.” 


Ndiyo kusema hata haya makambi ni hosteli za shule za kutwa tu kama shule iwe ya msingi ama sekondari Bodi/ kamati imekubaliana na wazazi imepata kibali kutoka kwa Bwana/ Bibi Mkurugenzi hilo halipaswi kuingiliwa na yoyote yule. Kwa mujibu wa kazi za kila mmoja mfano wa Wizara Elimu ina majukumu matano ambayo nni kutoa nyaraka, kutenga fedha, kutenga fedha na kutenga fedha. Kama kuna shida katika waraka nambari 3, 2016 wa Elimu Bure wanapaswa kutoa waraka mwingine na siyo kutoa maagizo.


Nimalizie kwa majukumu ya Wazazi na Walezi kulingana na barua hii yenye kurasa 10 na iliyosainiwa na Profesa Eustella Bhalalusesa ambaye alikuwa Kamishina wa Elimu.

3.10.III ya waraka inasema:


“Wazazi / Walezi watakuwa na majukumu la kushirikiana na uongozi wa shule kutoa chakula cha mchana kwa shule za kutwa na zenye hosteli kulingana na mazingira yao. Makubaliano yapelekwe kwa Mkurugenzi Mtendaji ili kupata kibali.” 


Ndiyo kusema kupiga marufuku masomo ya ziada ni kwenda kinyume na waraka wa elimu nambari 3 wa mwaka 2016 kwa kuwa hawa walimu wa ziada wa masomo ya sayansi na hisabati inawezekana wakapatikana wakati wa likizo.Ndiyo atakuwa nafasi pengine kwa mfano yeye anasomesha Shule ya kulipia ya Mazinde Juu, likizo atakuja kuwasomesha wanafunzi wa Ubiri na Shambalai sekondari za serikali Wilayani Lushoto. Kwa Wazazi wataelezwa watachangia pesa ya kumlipa mwalimu huyu, fedha ya chakula cha watoto wao pia itachangiwa na wazazi/walezi na masomo yanafanyika vizuri, wakifanya mtihani wa taifa watoto wetu wa shule hizi watafaulu kama wanafunzi wa Mazinde Juu. Muda wa likizo utatumika kuziba mapengo ya katikati ya mwaka.


Sasa ninaweka kalamu yangu chini kwa maeno ya rafiki yangu Philbert Masele kuwa 

“Katika biashara jambo uliloshindwa kulifanya leo, utalifanya kesho. Lakini katika masuala ya familia lile unaloshindwa kulifanya leo ndiyo kwaheri.” Neno hili liwe la hamasa kwa wazazi wenzangu kuchangia elimu za watoto wetu.Lakini pia Serikali inawajibu wa kulitupilia mbali katazo la masomo ya ziada.

Nasema siku nyengine.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI