Wafipa ni kabila linalopatikana katika eneo ambalo kijiografia ni pembe ya kando kando ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa ambapo kwa takwimu za awali zilizokusanywa na Wajerumani kati ya mwaka 1908-1909 kabila hili walikuwa ni watu 50,000. Katika kumbukumbu za Wajerumani za 1923 zikitaja Wafipa walikuwa 93,000 lakini baadaye Wajerumani hao wakasema kuwa Wafipa walilikuwa ni 68,000.......Na ADELADIUS MAKWEGA MBAGALA.
Kati ya mwaka 1931 takwimu zilionesha kuwa kabila hili lilikuwa na watu 44,172 na kwa eneo lote ukichanganya na wafipa na makabila mengine katikia ukanda huo walikuwa watu 53,311. Mwaka 1948 Wafipa walikuwa 61,248 wakati wakaazi wote katika ukanda huo walikuwa 78,252 na kwa mwaka 1958 Wafipa walikuwa 68,260 na wakaazi wote katika ukanda huo walikuwa 86,462. Msomaji wangu hizo takwimu zisikupe shaka kumbuka haya mambo ya zamani karibu miaka mia sasa.
Katika uchambuzi wa takwimu hizo ni kuwa katika mwaka 1957 Wafipa walikuwa ni 21.5 kwa kila maili za mraba. Ambapo ulikuwa na kuongezeka kwa makabila mengine kufika ukanda huo wa Ufipani. Kati ya mwaka 1948-1957 ilikuwa ni kwa asilimia 33.8 ya ongezekeo la wageni.
Wafipa ni miongoni mwa makabila ya kibantu ambao wanaishi Kusini mwa Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Rukwa. Katika eneo hilo wapo Wafipa, Wanyamwanga, Waiwa, Walungu(Warungu), Wapimbwe Wamambwe, Wawanda, Walungwa na Wakuulwe.
Wafipa ni kabila ambalo wanazungumza Kifika(Cifipa) ambacho wataalamu wa lugha wanadai wana Voweli saba (a, e, I, o,u). Katika kundi hilo wapo Wamambe, Walungu, Wapimbe na Walungwa (Rungwa). Wafipa pia na wanazungum wa lugha ya Kiswahili tangu enzi huku ikiwa ni lugha yao ya pili hasahasa kwa watu wazima wakike kwa wakiume.
Kama yalivyo makabila mengi ya kibantu ndugu hawa pia wamekuwa na utani miongoni mwao na makabila mengine. Mtu ambaye anafanya utani na mwenzake kwa kifipa wanasema Uwamwiko na chako/Uwanongwa wako akimaanisha wale wanaotaniana. Katika kundi hili wapo makabila ya Walunguru, Wabembe, Wangoni, Wanyamwezi, Wahehe na Wanyakyusa.
Chanzo cha utani wa Wafipa na makabila haya kinaaminika kuwa kilianza tangu mwaka 1798 ambapo wafipa walipata misukosuko mingi katika eneo hilo na makabila hayo niliyoyataja ambayo yalipita katika eneo hilo kwa nyakati tofauti kwa kuwavamia kivita.
Wangoni walipita katika ukanda huu wa Wafipa kutokea Afrika ya Kusini kwa kupitia Malawi (Nyasaland) huku wakiongozwa na kiongozi wao aliyefahamika kama Sungandaba. Kiongozi huyu wa Wangoni alikuwa na ndugu zake wawili Mpelembe na Mpenzeni huku wakipigana vita katika kila eneo walilopita kwa Wafipa, na kwa bahati njema Wangoni walishinda vita hivyo na kuwaita Wafipa watani kwa kuwa hawakuwa kikwazo kwao kupita.
Pia alikuja bwana mmoja aliyefahamika kama Kimalaunga aliyetokea huko Umakua alipita Songea, akapita Uhehe Iringa. Huyu Kimalaunga alifika kwa Chifu Mkoma wa Unyamwanga akampiga vizuri na mwisho alifika huko Unyamwanga akaweka makazi yake. Maeneo yote hayo ya Songea, Iringa alipigana vita na kushinda, huyu Mmakua alipofika kwa Chifu Mkoma baada ya kumpiga akaweka makazi huku watu wengi wa Chifu Mkoma wakijificha katika makaburi ambayo yalichimbwa kama mahandaki ili kuogopa kuteshwa na ndugu huyu. Baadaye inaaminika alifariki akiwa ameshafika Ufipani watu wengi waliposikia Kimalaunga amefariki ndipo wakatoka kutoka mafichoni na eneo hilo la Unyamwanga na Ufipa wakawa na amani.
Pia katika eneo hilo la ufipa alipita Chifu Kingalu ambaye aliweza kuwapiga vilivyo Wafipa, Wanyakiyusa na Wasafwa. Pia hata Chifu Mwambo wa Tabora aliweza kupita ufipani kupata maeneo zaidi na hilo likaleta utani baina ya Wafipa, Waluguru na Wanyamwezi.
Kama tulivyoona ndugu hawa wanafanya utani na makabila swali ni je Wafipa hawana utani miongoni mwao wenyewe? Kulijibu swali hilo, ni kuwa kweli wafipa wanao utani wa wenyewe kwa wenyewe. Kwanza utani wa Binamu na Binamu. Samahani kwa msomaji nitatumia maneno makali na Ashakumu si Matusi. Kwa mfano. Mpumbavu, Kumanyoko, nsuti yako(sehemu ya siri ya mwanaume), nyoko-sehemu ya siri ya mwanamke, mbwa usinda(mkia wa mbwa).
Pia kuna utani baina ya wazazi walioleana yaani baba na mama wa kila upande hawa huwa ni watani wanaitwa Kayemba. Pia kuna utani baina ya mjomba na mtoto wa dada yake yaani mpwa ambapo utani huo unaitwa Mambwe.
Mahusiano ya kibinamu kwa Wafipa hayaonekani kama ni ya damu sana kwa hiyo wafipa mabinamu hao wanaweza kufunga ndoa hata kulala pamoja na katika hilo hakuna wa kuhoji. Wanamsemo kuwa Binamu Inyama ya hamu. Hapa kama ndoa ikitangazwa hakuna wa kulipinga. Kumbe na mimi ninayeandika nina binamu zangu Wafipa kumbe ningetangaza ndoa na binamu zangu.
Mahusiano baina ya wazazi ambao watoto wao wameona utani pia ni jambo la kawaida kama nilivyokwambia hapo juu yanaitwa Kayemba kwa kuwa watoto wao wamefunga ndoa kila upande unatambua siri za upande wa pili, utani haukwepeki.
Naomba kwa leo niiweke kalamu yangu chini lakini ninaomba radhi sana kwa kutumia maneno makali ni kwa nia ya kufundisha tu jamii hasa kujua kile kilichomo katika kabila hilo la WAFIPA. Nakukumbusha tu kama una binadamu yako Mfipa na unataka kuoa/kuolewa naye hilo ruksa, mie hilo sikulijua mwanakwetu! maana nina binamu zangu wakike Wafipa watatu na wameshaolewa kwa hiyo nimeula wa chunya. Nakutakia siku njema.
Makwadeladiusa@gmail.com
0717649257
0 Comments