JUMLA ya shilingi bilioni 22.689, zimetengwa na Serikali Kuu kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizoko mkoa wa Kilimanjaro kwa mwaka wa fedha 2021/2022, ambapo kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 13.9 ni fedha za miradi ya maendeleo kutoka serikali kuu na shilingi bilioni 8.7 fedha za matengenezo kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund Board). mwandishi wa matukio daima Rehema Abraham anaripoti kutokea Kilimanjaro
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai, ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi na matengenezo ya barabara kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA).
"Serikali imetenga jumla ya shilingi 22,689,111,449.19; miradi itakayotekelezwa kupitia fedha hizi na kukamilika itawaondolea wananchi kero zinazotokana na kuweko kwa barabara zisizopotika", alisema.
Amesema “Serikali mkoani Kilimanjaro tumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kiwango cha fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara mkoani kwetu,”alisema Kagaigai.
Amesema jumla ya zabuni 68 zimetangazwa na katika awamu ya kwanza ambapo makandarasi 28 walipatikana kwa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 6,079,593,710.66.
Aliongeza, "Nitoe rai kwa Wakandarasi mliokabidhiwa jukumu la kutekeleza miradi hii kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kupunguza adha ya wananchi ambao wamekuwa wakishindwa kupita wakati wa msimu wa mvua,”alisema.
Ameelezea matumaini yake ya kuwa wakandarasi hao watatekeleza miradi hiyo kwa viwango vya ubora na ufanisi ule unaotakiwa na kwamba thamani ya fedha iliyowekwa kwa ajili ya miradi hiyo itaonekana.
Awali katika taarifa yake, Meneja wa TARURA Mkoani Kilimanjaro Mhandisi Nicholas Francis, amesema jumla ya mikataba 14 imesainiwa katika hafla hiyo.
"Hafla hii ya utiaji saini mikataba ni ya awamu ya pili kwa mwaka huu wa fedha wa 2021/2022, ikitanguliwa na ile ya awamu ya kwanza ambapo jumla ya mikataba 28 ilisainiwa", amesema.
0 Comments