Header Ads Widget

WAZALISHAJI WA ZAO LA MTAMA WAONGEZEKA

MPANGO wa Chakula Duniani (WFP), kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ireland (Irish Aid) wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya Mtama kwa msimu wa mwaka 2020/2021, ambapo wakulima wamezalisha zaidi ya tani 17,000 za Mtama na kuweza kujipatia kiasi cha shilingi bilioni 9. mwandishi wa matukio daima Rehema Abraham anaripoti kutokea Kilimanjaro.

Mkuu wa Ofisi ndogo ya WFP, Neema Mina Sitta, aliyasema hayo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema zaidi ya wakulima 22,000 wa zao la Mtama kutoka wilaya za Kongwa, Bahi na Mpwapwa wamefanikiwa   kuuza tani 17,000 za zao hilo kwa msimu wa mwaka 2020/2021.

“Kupitia mpango huu wakulima wa zao la Mtama wamenufaika na kilimo hicho kupitia Program ya Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), inayotekelezwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kupitia Mpango Mkakati wa 2017 hadi 2022 wameweza kunufaika na kilimo hicho,”alisema 

Sitta alisema WFP iliandika mradi wa kilimo himilivu katika wilaya za mkoa wa Dodoma na kupata ufadhili wa Shilingi bilioni 1.7 kutoka Shirika la Maendeleo la Ireland (Irish Aid) ambapo matunda yameshaonekana kwa wakulima zaidi 22,000 kujipatia kiasi cha Shilingi bilioni 9.

Alisema uamuzi wa WFP kuingia katika Kilimo Himilivu cha Mtama wameweza kuunganisha wakulima na soko moja kwa moja na kuondoa madalali au watu wa kati na walikuwa wanachangia kushusha bei ya zao.

Mkuu huyo alisema kuwa kwa sasa bei ya zao la mtama kilo moja inaunzwa hadi Shilingi 550 kutoka Shilingi 250 ya awali hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na kuhamasisha kilimo hicho.

Sitta, aliongeza kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima namna ya kulima kilimo bora na endelevu ambacho kitaweza kuwaingizia mapato yao na nchi kwa ujumla.

Sambamba na hayo msimu ujao (WFP), wanatarajia uzalishaji wa zao la Mtama utaongezeka kutokana na kuongezeka kwa wilaya za  Chemba, Kondoa, Dodoma na Chamwino.

Katika hatua nyingine alisema wamepokea ombi la Serikali katika kuanzisha program za kuongeza uzalishaji kwenye zao la alizeti ambapo matarajio yao ni kuingiza kwenye Mpango Mkakati wa WFP wa 2022 hadi 2027.

Aidha, WFP imekuwa ikinunua mazao mengine kama vile mahindi kwa ajili ya kupeleka katika ofisi za WFP za nchi nyingine na kwenye kambi za wakimbizi za nduta na Nyarugusu.

Hata hivyo WFP ni mpango ambao unafanya kazi kwa mtazamo wa kibinadamu kama kusaidia Sekta ya Kilimo, Maendeleo, Wakimbizi, Afya na Lishe ambapo kwa mkoa wa Dodoma wameweza kusaidia wakulima wa zao la mtama na kuongeza uzalishaji

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI