Akizungumza katika mkutano wa hitimisho wa mradi huo jana Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tabora anayeshughulikia Rasilimali watu Hamis Mkunga alisema mradi huo umeboresha utoaji huduma za afya kwa kiasi kikubwa katika afua mbalimbali.
Alisema kwamba mradi wa Tuimarishe afya katika kipindi cha miaka 2 waliweza kuwajengea uwezo timu za waratibu wa huduma za Bima ya Afya iliyoboreshwa jambo ambalo limepelekea kuongeza idadi ya wanachama wa mfuko huo.
Hamis Mkunga alitaja Manufaa mengine ni kuimarisha mfumo wa taarifa za Bima ya afya iliyoboreshwa, kuwajengea uwezo Maafisa Afya, Wataalamu wa Vifaa Tiba na Timu za Afya za Mikoa hiyo (RHMT).
Aidha aliwataka Makatibu Tawala wa Mikoa hiyo, Waganga Wakuu (RMO’s) na Wataalamu wa Afya kusimamia na kuendeleza yale yote yaliyofanywa na mradi huo.
Awali Mtaalamu Mshauri wa Mradi huo Emanuel Mwanga alisema kuwa kupitia mradi huo huduma mbalimbali za afya zimeboreshwa katika Mikoa hiyo ikiwemo kuziongezea weledi timu za afya, kuboreshaa vifaa tiba na mifumo ya uratibu wa ICHF iliyoboreshwa.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Geofrey Maleale alishauri Uongozi wa Mikoa hiyo kushughulikia changamoto za afya zilizopo katika maeneo yao ambazo hazikumalizwa na mradi huo.
Mradi huo wa kimkakati wa miaka 2 uliotekelezwa na serikali ya Tanzania kwa ushirikano na serikali ya Uswisi tangu Novemba 2019 hadi Oktoba 2021 umewajengea uwezo mkubwa wataalamu wa afya na kuanza kutoa huduma bora kwa jamii.
0 Comments