Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma
TANZANIA imeeleza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wa kijeshi na kuimarisha mifumo ya usalama wa pamoja barani Afrika, huku ikizitaka nchi za bara hilo kuwekeza katika elimu na mafunzo ya kijeshi yatakayowaandaa viongozi kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazobadilika.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), wakati akifunga Mkutano wa 20 wa Makamanda wa Vyuo vya Ukamanda na Mafunzo ya Kijeshi barani Afrika (African Conference of Commandants – ACoC), uliofanyika Novemba 11, 2026, jijini Arusha.
Dkt. Nyansaho amesema kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za kijeshi za nchi za Afrika ni muhimu katika kujenga uwezo wa pamoja wa kukabiliana na vitisho vinavyoathiri usalama wa mataifa, ikiwemo ugaidi, uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka na vitisho vya kimtandao.
Amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia misingi ya Umoja wa Afrika, usalama wa pamoja na ushirikiano wa kikanda ili kuchangia juhudi za kudumisha amani na utulivu wa kudumu barani humo.
Katika hotuba yake, Dkt. Nyansaho aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa makamanda na wajumbe walioshiriki mkutano huo.
Aidha, aliwapongeza washiriki kwa michango yao katika kujadili namna bora ya kuimarisha elimu ya kijeshi na ushirikiano baina ya vyuo vinavyotoa mafunzo ya ukamanda na uongozi wa kijeshi barani Afrika.
Alibainisha kuwa elimu na mafunzo ya kitaaluma ya kijeshi yana mchango mkubwa katika kuandaa viongozi wenye maarifa, maono na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama.
Alisisitiza umuhimu wa vyuo vya kijeshi kushirikiana zaidi kupitia mafunzo ya pamoja, kubadilishana wanafunzi na wakufunzi pamoja na kuoanisha mitaala ya mafunzo ili kuongeza ufanisi na kujenga uelewa unaofanana katika masuala ya kiusalama.
Alitaja maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele kuwa ni Operesheni za Kusaidia Amani, Sheria za Kimataifa za Kibinadamu na Ulinzi wa Raia, ambayo alisema ni sehemu muhimu ya maandalizi ya majeshi katika kutekeleza majukumu yake.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali waandamizi wa kijeshi kutoka mataifa ya Afrika, akiwemo Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salumu Haji Othman, pamoja na Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Tanzania na Mwenyekiti wa Mkutano wa Makamanda wa Vyuo vya Kijeshi vya Afrika (ACoC), Meja Jenerali Stephen Justice Mnkande.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, wawakilishi wa Umoja wa Afrika, makamanda wa vyuo vya kijeshi, wakufunzi wakuu na maafisa waandamizi wa kijeshi.
Mkutano huo umetumika kama jukwaa la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za mafunzo ya kijeshi, kwa lengo la kuongeza uwezo wa majeshi ya Afrika kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za kiusalama na kuendeleza juhudi za kulifanya bara hilo kuwa na amani na utulivu wa kudumu.













0 Comments