Na Matukio Daima Media, Morogoro.
Mkoa wa Morogoro unakuwa mwenyeji wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA) 2026, yatakayowakutanisha washiriki zaidi ya 4,000 kutoka taasisi, mashirika ya umma na makampuni binafsi, katika michezo 13 itakayofanyika kwenye viwanja mbalimbali vya mji huo.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kufungua mashindano hayo Novemba 12 mwaka huu,kwa niaba ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ambaye ni mlezi wa SHIMMUTA.
Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu anatarajiwa kushuhudia mchezo wa kuvuta kamba utakaokuwa sehemu ya matukio ya ufunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Katibu Mkuu wa SHIMMUTA, Dkt. Maswet Masinde, amesema mashindano ya mwaka huu yamezingatia ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalum kwa kuwajumuisha katika michezo ya karata, bao, pool table na draft kulingana na mahitaji yao.
Amesema katika hafla ya ufunguzi, Waziri Mkuu ataambatana na Naibu Waziri wa Michezo, Hamis Mwinjuma, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa.
Historia ya SHIMMUTA inaanzia mwaka 1967, yalipoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza michezo na mshikamano miongoni mwa watumishi wa mashirika na taasisi mbalimbali.
Dkt. Masinde amesema uwepo wa washiriki zaidi ya 4,000 unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Morogoro, hususan katika sekta za hoteli, migahawa, usafiri na biashara ndogondogo.
Ameeleza kuwa uamuzi wa kutumia Mkoa wa Morogoro kama Mwenyeji wa Michuano hii ulitokana na ombi la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima, ambaye kwa sasa anaongoza Mkoa wa Lindi.
Mwisho






0 Comments