Na,Jusline Marco:Arusha
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki imetakiwa kuimarisha utoaji wa haki, kuharakisha utatuzi wa migogoro ya kibiashara na kuhakikisha maamuzi yake yanatekelezwa na Nchi Wanachama ili kuchochea biashara na uwekezaji katika ukanda huo.
Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, ambapo taasisi hiyo ina nafasi muhimu katika kulinda Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuhakikisha nchi wanachama zinafuata makubaliano yaliyowekwa.
Akizungumza jijini Arusha katika maadhimisho hayo,Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda Rebecca Kadaga, amesema Mahakama hiyo haipaswi kuwa chanzo cha kukwamisha maendeleo ya kiuchumi kupitia migogoro ya muda mrefu, bali inapaswa kuhakikisha wafanyabiashara na wawekezaji wanapata haki kwa wakati na kwa misingi ya usawa.
Aidha amesema kuwa ustawi wa kiuchumi wa Afrika Mashariki unategemea uzalishaji wa bidhaa na huduma pamoja na kuwepo kwa soko kubwa la pamoja litakalowezesha bidhaa hizo kuuzwa katika nchi zote wanachama ambapo kuimarika kwa soko hilo kutatoa fursa kwa wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji kupanua shughuli zao na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa ukanda huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Stephen Mbundi amehimiza kuimarishwa kwa uwezo wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kwa kuipatia rasilimali za kutosha, teknolojia na wataalamu ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki na utatuzi wa migogoro ndani ya Jumuiya hiyo.
Amesema tangu kuanzishwa kwake mahakama hiyo imeendelea kuwa chombo muhimu katika kutafsiri na kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo ameeleza kuwa hadi kufikia Agosti 2026, mahakama hiyo ilikuwa imesajili jumla ya mashauri zaidi ya 1000, hali inayoonesha kuongezeka kwa umuhimu na utambuzi wake katika kutatua migogoro inayohusu utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Wakili Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ally Possi, amesema Tanzania ni miongoni mwa wadau wanaoshiriki katika uendeshaji wa mashauri ya mahakama hiyo, hivyo ina wajibu wa kuhakikisha taasisi hiyo inachangia maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia ina nafasi muhimu katika shughuli za Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kwa kuwa ni mwenyeji wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na mahakama hiyo imekuwa ikiendesha shughuli zake jijini Arusha.
Naye Rais wa Mahakama hiyo,Jaji Nestory Kayobera katika hotuba amesema utekelezaji wa hukumu za Mahakama ni muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria, uwajibikaji na imani ya wananchi katika mfumo wa haki wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu, taratibu na maamuzi ya Mahakama kupitia elimu ya sheria, majukwaa ya kidijitali na ushirikiano na Mahakama za kitaifa, vyama vya wanasheria, vyuo vikuu na vyombo vya habari.
Maadhimisho hayo ya miaka 25 yanalenga kutambua mchango wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki katika kuimarisha haki, sheria na ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ambapo yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Kutoka Misingi Imara kuelekea Mustakabali,” yakilenga kutafakari mafanikio ya Mahakama hiyo katika kipindi cha miaka 25 na kuweka mikakati ya kuimarisha nafasi yake katika maendeleo ya kikanda.










0 Comments