Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema kuwa ushirikiano wa Marekani na taifa lake katika kutoa taarifa za kijasusi kuhusu mashambulizi hatari ya makombora ya Urusi sasa umeanza kufanya kazi, baada ya kufanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff.
Mkutano huo ulifanyika mjini Oslo, kufuatia tuhuma za Ukraine kwamba Washington ilikuwa imesitisha kutoa taarifa muhimu za kijasusi madai ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliyakataa na kuyataja kuwa uongo.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema mfumo huo umeanza tena kufanya kazi kwa ufanisi.
"Tunashukuru kwamba mifumo ya ujasusi inafanya kazi. Ninazungumzia mifumo ya tahadhari ya mapema, ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wetu, watoto, watu wazima na raia kwa ujumla, kwa sababu tunaweza kupata taarifa ya tahadhari wakati kombora la masafa marefu linapokuja. Ukraine inataka amani kuliko mtu mwingine yeyote. Na ni Urusi ndiyo iliyoanzisha vita hivi. Uamuzi wa kuendeleza mauaji ni wa Urusi, na Urusi pekee ndiyo inayopaswa kuwajibika kwa uamuzi huo.’’
Rais wa Finland, Alexander Stubb, ambaye pia alishiriki katika mazungumzo hayo, alisema kuwa wamepiga hatua kuhusu mapendekezo ya kufikia amani, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, bado hajatoa maoni yake hadharani kuhusu mapendekezo hayo ya hivi karibuni.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema kuwa Kremlin itasikiliza mapendekezo ambayo Witkoff atawasilisha, huku akiondoa uwezekano wa “makubaliano yoyote ya kisiasa yanayohusisha kufanya mapatano kwa upande wa Urusi”.






0 Comments