Na Elamu Nyaulingo (UoI), Matukio Daima Media, Iringa
Baadhi ya wananchi mkoani Iringa wamelalamikia vitendo vya udanganyifu vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya madalali wa nyumba za kupanga, wakisema wanakabiliwa na gharama zisizoeleweka, maelezo yasiyo sahihi kuhusu nyumba na kuonyeshwa makazi yasiyolingana na matarajio yao.
Wakizungumza na Matukio Daima Media, wananchi hao wamesema changamoto hizo zinawapelekea kupata usumbufu na hasara za kifedha wanapotafuta makazi, huku wakitaka madalali kuzingatia uaminifu, uwazi na kutoa taarifa sahihi kabla ya makubaliano ya upangaji.
Mmoja wa wananchi hao, Moses Idd, amesema baadhi ya madalali hudai malipo ya ziada ambayo hayakuelezwa mwanzoni, hali inayoongeza gharama za kupata nyumba za kupanga.
“Unakuta mtu anatafuta chumba cha Shilingi 50,000 kwa mwezi, lakini anadaiwa fedha nyingine za udalali ambazo hakuambiwa tangu mwanzo,” amesema Idd.
Kwa upande wake, Nelson Damasi Mbilinyi, mkazi wa Iringa, amesema amekumbana na changamoto ya kuonyeshwa nyumba ambazo maelezo yake hayaendani na hali halisi, akibainisha kuwa baadhi ya nyumba huonekana kuwa na huduma nzuri wakati wa kuzitafuta, lakini baada ya mpangaji kuhamia hugundua kasoro mbalimbali.
Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni nyumba kuingiza maji wakati wa mvua, pamoja na tofauti kati ya eneo aliloelezwa na dalali na eneo ambalo nyumba husika ipo.
Marianna Kalinga amewashauri wananchi kuwa makini wanapotafuta nyumba za kupanga kwa kuhakikisha wanazikagua kabla ya kufanya malipo na kuthibitisha upatikanaji wa huduma muhimu, pamoja na masharti ya upangaji.
“Ni muhimu mtu akague nyumba kabla ya kulipia na kuhakikisha anakubaliana na mwenye nyumba kuhusu kodi na masharti ya upangaji,” amesema Kalinga.
Ili kupunguza changamoto hizo, wapangaji wanashauriwa kuthibitisha eneo la nyumba, kukagua hali yake na huduma za maji na umeme, pamoja na kuelewana mapema kuhusu kodi, amana na ada ya udalali.
Aidha, wanapaswa kudai risiti za malipo na kusoma kwa makini mkataba wa upangaji kabla ya kuusaini, hatua zinazoweza kusaidia kupunguza hasara na migogoro kati ya wapangaji, wamiliki wa nyumba na madalali.






0 Comments