Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema hahitaji msaada wa nchi nyingine katika kukabiliana na Iran, akisisitiza kwamba Marekani ina uwezo wa kushinda mgogoro huo peke yake.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House Jumanne jioni, Trump alirudia madai yake kuhusu ubora wa Marekani katika mvutano unaoendelea na Iran.
"Kama mnavyojua, tunaendelea vizuri sana kuhusu Iran. Kilichobaki ni kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu namna tutakavyoshinda; je, tutafanya hivyo kwa njia ya amani au kwa njia kali?" alisema Trump.
Aliongeza kuwa: "Kwa vyovyote vile, tunaendelea vizuri sana na hatuhitaji msaada wa mtu yeyote."
Akizungumzia kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia vikwazo vya usafiri katika Mlango wa Hormuz, Trump alisema wananchi wengi hawajaridhishwa na gharama za mafuta, lakini akaeleza kuwa hiyo ni gharama ndogo ikilinganishwa na hatari ya Iran kupata silaha za nyuklia.
"Watu hawafurahishwi na bei ya mafuta. Hata hivyo, hiyo ni gharama ndogo kulipa ili kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia," alisema.
Trump pia alisema aliwasiliana na viongozi wa nchi mbalimbali ili kubaini kama wangekuwa tayari kuisaidia Marekani, lakini alidai kuwa wote walikataa.
"Nilikuwa nawajaribu tu. Niliwapigia marais na mawaziri wakuu kadhaa kuwauliza kama wangependa kutusaidia, na wote walisema hapana," alisema.
Hata hivyo, hakutaja viongozi aliowasiliana nao wala maelezo ya mazungumzo hayo.
Kauli hizo zinakuja saa chache baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuchapisha video ya mazungumzo yake ya simu na Trump. Katika video hiyo, Netanyahu anasikika akisema:
"Donald, bado tuna kazi ambayo haijakamilika. Tutaikamilisha pamoja kwa sababu hakuna mwingine anayeweza kufanya hivyo."
Wakati huo huo, Iran imeendelea kushinikiza kusitishwa kwa vitisho kutoka Marekani na Israel. Siku moja iliyopita, Tehran iliwasilisha barua kwa Umoja wa Mataifa ikitaka hatua zichukuliwe kukomesha vitisho hivyo.
Maafisa waandamizi wa Iran pia walisisitiza katika mazungumzo yao na mkuu wa jeshi la Pakistan, Asim Munir, kwamba sharti la kuanza tena mazungumzo na Marekani ni Washington kuheshimu masharti yaliyofikiwa katika makubaliano ya Islamabad.






0 Comments