Na Matukio DaimaMedia
Kampuni ya Tripbey imezindua mfumo wa huduma za usafiri unaowawezesha wananchi kupata tiketi za ndege, mabasi na treni bila kulipa nauli kabla ya kuanza safari, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Balozi wa Tripbey, Maulid Kitenge, amesema huduma hiyo inawawezesha watumiaji kuomba tiketi kupitia programu ya simu ya kampuni hiyo na kulipa gharama za safari baadaye, kwa kuzingatia masharti na vigezo vilivyowekwa.
Kitenge amesema mfumo huo unalenga kuwapa wananchi unafuu katika kupanga safari zao, hususan wale wanaohitaji kusafiri kwa dharura au ambao hawana fedha za kutosha kulipia nauli mara moja.
Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa huduma hiyo, kampuni inatumia mfumo wa kutathmini uwezo wa kifedha wa mtumiaji, unaojulikana kama Ability to Pay, ili kubaini uwezo wake wa kulipa gharama za safari baada ya kupata huduma.
Amesema tathmini hiyo inalenga kuhakikisha wanaopata fursa ya kutumia mfumo huo wanakidhi vigezo vya kifedha vilivyowekwa na kuzingatia masharti ya ulipaji wa nauli baada ya safari.
Kwa mujibu wa Kitenge, huduma hiyo inahusisha usafiri wa ndege za ndani, mabasi ya mikoani na treni, jambo linalowapa wananchi machaguo mbalimbali ya kupanga safari zao kulingana na mahitaji yao.
Kwa upande wake, Afisa Masoko na Uendeshaji wa Tripbey, Idrisa Njeru, amesema kampuni hiyo inatumia teknolojia ya kidijitali kurahisisha mchakato wa kupata tiketi na kutoa njia mbadala ya malipo ya usafiri.
Njeru amesema mfumo huo unawawezesha watumiaji kupata huduma ya usafiri kwanza na kulipa baadaye, kwa mujibu wa masharti yanayoambatana na huduma hiyo.
Hata hivyo, amewashauri wananchi wanaotaka kutumia huduma hiyo kufahamu masharti ya malipo, vigezo vya kustahiki na gharama zinazoweza kuhusishwa na huduma hiyo kabla ya kuwasilisha maombi ya tiketi.



.jpeg)





0 Comments