NA AMINA SAIDI, TANGA.
Sekta ya kilimo nchini imeingia katika sura mpya kufuatia kuibuka kwa teknolojia mpya ya uzalishaji wa mbolea ya miamba pamoja na kuongezeka kwa hamasa ya utekelezaji wa kilimo ekolojia hai, hatua inayolenga kurejesha rutuba ya udongo, kulinda afya za walaji, na kufungua fursa mpya za masoko ya kimataifa.
Akitambulisha teknolojia hiyo mpya mkoani Songwe, mgunduzi wa mbolea ya miamba, Donald Mwakamele, ameeleza kuwa mbolea hiyo imetengenezwa kwa kutumia miamba pekee bila kuchanganywa na kemikali yoyote, lengo likiwa kurejesha udongo katika uasilia wake na kuupatia virutubisho vyote muhimu pamoja na vitamini vinavyohitajika na mimea.
Makame alibainisha kuwa tofauti na mbolea za kawaida zinazomlazimisha mkulima kununua kila msimu, mbolea hii ya miamba ina uwezo wa kudumu udongoni kwa muda wa miaka mitatu, hatua inayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji kwani mkulima ana uwezo wa kulima na kuvuna kwa kipindi chote hicho bila kuweka mbolea tena.
Kiwanda cha mbolea hiyo kilichopo mkoani Songwe tayari kimefunguliwa na kuanza uzalishaji, huku matokeo chanya yakianza kuonekana katika maeneo mbalimbali kama vile Moshi, Njombe, na Songea ambako mbolea hiyo imefanya vizuri katika kuboresha mazao na kurudisha madini halisi ya ardhi.
Kwa upande wake Afisa Mhamasishaji Paul chilewa kutoka Mtandao wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), akizungumza mkoani Tanga katika Maonyesho ya Siku ya Chakula Duniani, amewahimiza wakulima nchini kuchangamkia na kutumia pembejeo hai ili kulinda afya za walaji na kuongeza tija kwenye udongo.
Chilewa alieleza kuwa (TOAM), kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wengine, wanaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kilimo Ekolojia Hai wa mwaka 2023–2030, ambao kipaumbele chake kikuu ni kuhakikisha pembejeo hai ikiwemo mbolea hai, viuatilifu hai, na mbegu za asili zinawafikia wakulima kwa urahisi na kwa wakati.
Akionya kuhusu athari za viuatilifu vya kemikali, alibainisha kuwa matumizi yake yamekuwa yakiacha mabaki ya sumu kwenye mazao kama vile maembe na matunda mengine, jambo linalohatarisha afya ya jamii na kusababisha magonjwa sugu kama matatizo ya figo yanayogharimu fedha nyingi kutibu.
Alihitimisha kwa kueleza kuwa matumizi ya pembejeo za asili yatawezesha mazao ya Tanzania kuingia kwa urahisi katika masoko ya kikanda na Ulaya ambako bidhaa zisizo na kemikali zina mahitaji makubwa, ikiwa ni sehemu ya kufikia Dira ya 2050 yenye lengo la kuwa na jamii yenye afya bora, kilimo chenye tija, na maisha endelevu.






0 Comments