Header Ads Widget

MASOKO NA MAGHALA, KIKWAZO KWA VIJANA WANAOKIMBILIA KILIMO


Matukio Daima, Morogoro

LICHA ya kilimo kuanza kuwapa vijana fursa za kujiajiri na kujenga biashara, upatikanaji wa masoko ya uhakika na maghala ya kuhifadhi mazao ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kutatuliwa ili kuwawezesha kunufaika zaidi na shughuli hizo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amesema vijana wanapaswa kutafuta soko kabla ya kuanza uzalishaji ili kupunguza hatari ya kuuza mazao kwa madalali na kupoteza sehemu ya faida. 

Pia ameiomba Wizara ya Kilimo na wadau wengine kuongeza juhudi za kujenga maghala na kuwaunganisha wakulima na masoko makubwa ya mpunga.

Wito huo unakuja wakati vijana wanaonufaika na Mpango wa Vijana Kilimo Biashara wakieleza namna ujuzi na zana walizopata zinavyowasaidia kuboresha shughuli zao. 

Fadhili Machela wa Dumila, Wilaya ya Kilosa, Jenipher Ndani wa Morogoro na Christina Chidau wa Gairo wamesema mpango huo umewapa fursa ya kujifunza, kujiunga katika vikundi na kutumia vifaa vya kisasa katika shughuli za kilimo.

Baadhi ya vifaa vinavyotumika katika shughuli hizo ni vya umwagiliaji, uzalishaji wa miche na upuliziaji wa viuatilifu, vinavyolenga kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kuwasaidia vijana kuendesha kilimo kwa mtazamo wa kibiashara.

Mkuu wa Mnyororo wa Ugavi na Lojistiki wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Mahmoud Mabuyu, na Mratibu wa Building Better Tomorrow (BBT), David Josphat, wameeleza umuhimu wa kuwawezesha vijana kujenga uwezo wa kuendesha biashara zinazotokana na kilimo, kupitia ushirikiano wa wadau.

Mpango huo unaohusisha WFP, Mastercard Foundation, BBT na Nafaka Kilimo umefikia vijana 77,368 nchini tangu mwaka 2023, wakiwemo wanawake wanaochangia asilimia 50.2 ya wanufaika. Pia, biashara 1,451 za vijana zimepata msaada wa kuimarisha ujuzi wa biashara, elimu ya fedha, teknolojia na upatikanaji wa masoko.

Katika hatua nyingine, vijana 303 kutoka Morogoro na Dodoma wamekabidhiwa zana za kilimo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 220, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza tija na kupanua fursa za kujiajiri. Hata hivyo, upatikanaji wa masoko na miundombinu ya kuhifadhi mazao utaendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha uwezeshaji huo unaleta manufaa ya kiuchumi kwa vijana.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI