Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MAKAO ya Taifa ya Watoto Kikombo yameadhimisha kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kujumuika na watoto wenye uhitaji katika michezo, burudani na chakula cha pamoja, hatua inayolenga kuendeleza misingi ya upendo, umoja na mshikamano aliyoiacha kwa Watanzania.
Shughuli hizo zilizofanyika katika Hoteli ya Residence ziliwakutanisha watoto na wadau mbalimbali katika mazingira ya furaha, ambapo walipata nafasi ya kucheza, kufurahi na kula pamoja, huku wakikumbushwa umuhimu wa kuwajali na kuwathamini wengine katika jamii.
Akizungumza Jana October 14 Dodoma wakati wa shughuli hizo, Meneja wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo, Derive Kalijongo, amesema wameamua kutumia siku hiyo muhimu kwa kushirikiana na watoto katika michezo na burudani ili kuwapa furaha na kuwaonesha upendo.
Amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kuenzi kwa vitendo misingi ya kujali wengine na kuimarisha upendo katika jamii, ambayo ni miongoni mwa mambo yanayokumbukwa katika urithi wa Hayati Mwalimu Nyerere.
“Tumetoka na watoto kuwapa upendo na furaha, na hii yote ni katika yale aliyokuwa akifanya Baba wa Taifa kuhakikisha,” amesema Kalijongo.
Amesema kuwashirikisha watoto katika shughuli za kijamii kunatoa nafasi ya kujenga ukaribu nao na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza matendo yanayowaletea furaha.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Wakili Happy Msimbe, ameipongeza Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo kwa kuadhimisha kumbukizi hiyo kwa namna ya kipekee, akisema kitendo cha kuwashirikisha watoto katika michezo na burudani kinaonesha upendo unaotekelezwa kwa vitendo.
Msimbe amesema Hayati Mwalimu Nyerere alisisitiza misingi ya upendo, mshikamano, umoja na usawa, hivyo ni muhimu kwa jamii kuendelea kuenzi misingi hiyo kwa kuwajali watu wengine, wakiwemo watoto wenye uhitaji.
“Jambo mlilofanya ni la kipekee, kwani Hayati Baba wa Taifa alieneza upendo, mshikamano, umoja na usawa,” amesema.
Ameongeza kuwa amefurahishwa na namna kituo hicho kilivyoamua kuwakutanisha watoto katika shughuli za pamoja, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuendeleza na kuyaenzi mambo mema yaliyofanywa na Baba wa Taifa.
“Leo tuko hapa kumkumbuka Baba wa Taifa na tunayaenzi yale yote aliyokuwa akiyafanya hakika nimefurahishwa,” amesema Msimbe.
Naye Meneja wa Mradi wa Mfuko wa Abbott, Edna Hauli, amesema wameungana na watoto katika maadhimisho hayo kwa kushiriki chakula, vinywaji, michezo na burudani, ikiwa ni sehemu ya kukumbuka upendo aliokuwa nao Baba wa Taifa.
Hauli amesema siku hiyo imekuwa fursa ya kujumuika na watoto katika mazingira ya furaha na kuonesha umuhimu wa kuwa karibu nao kupitia shughuli zinazowapa nafasi ya kushiriki na kufurahia pamoja na wengine.
“Leo ni siku ya furaha, tunakumbuka upendo aliokuwa nao Baba wa Taifa,” amesema Hauli.
Maadhimisho hayo yameonesha namna kumbukizi ya viongozi wa kitaifa inavyoweza kuambatana na matendo ya kijamii yanayogusa maisha ya watu, hususan watoto wenye uhitaji, kwa kuendeleza upendo, utu na mshikamano katika jamii.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)







0 Comments