![]() |
| Jengo la Maabara la TMDA Kanda ya Mashariki, Mabibo Dar es salaam |
![]() |
| Baadhi ya vifaa tiba vilivyokutwa kwenye maduka hayo ambavyo vimekwisha tumika |
Na. Mwandishi Wetu, Dar.
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Mkoa Maalum wa Kikaguzi Temeke, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, imefunga maduka matano ya Dawa Muhimu baada ya kubainika kuwa yalikuwa yakitoa huduma za kitabibu kinyume cha Sheria na taratibu zilizowekwa.
Maduka hayo yamebainika kuwa yalikuwa yakitoa huduma za matibabu ambazo haziruhusiwi kutolewa katika maduka ya dawa, ikiwemo kuwachoma wateja sindano ndani ya maeneo ya biashara hizo.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ukaguzi maalum unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Temeke, unaofanywa na TMDA kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za dawa, Vifaa Tiba na bidhaa nyingine za afya zinatolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kitaaluma.
Mbali na utoaji wa huduma za kitabibu kinyume cha utaratibu, ukaguzi huo umebaini makosa mengine katika maduka hayo, ikiwemo kuyaendesha bila kuwa na vibali vinavyohitajika pamoja na kutumia watoa huduma wasio na sifa stahiki.
TMDA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria na kiudhibiti ili kulinda afya za wananchi dhidi ya utoaji wa huduma za dawa na vifaa tiba usiozingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kama ilivyobainishwa kwenye takwa la Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219.
![]() |
| Baadhi ya vifaa tiba vilivyokutwa kwenye maduka hayo ambavyo vimekwisha tumika |










0 Comments