Header Ads Widget

Japan MWANAJESHI WA MAREKANI AKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI NCHINI JAPAN

Mwanajeshi wa Jeshi la Majini la Marekani (US Marine) amekamatwa kwa tuhuma za kumuua mwanamke mmoja baada ya mwili wake kupatikana katika hoteli kwenye kisiwa cha Okinawa, kusini mwa Japan, kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo.

Waziri wa Japan, Sanae Takaichi, alilaani tukio hilo, akilielezea kuwa ni tukio la uporaji na mauaji ya "kikatili na ya kutisha". Alisema ameitaka Marekani kuimarisha usimamizi na nidhamu miongoni mwa wanajeshi wake waliopo nchini Japan.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la NHK, marehemu ametambuliwa kuwa Yagi Anna, mwenye umri wa miaka 39, huku mtuhumiwa akitajwa kuwa Devin Jacob Ballard, mwenye umri wa miaka 20. Ballard anahudumu katika Kituo cha Anga cha Jeshi la Majini la Marekani cha Futenma, kilichoko Okinawa.

Kamandi ya Jeshi la Majini la Marekani ilisema inashirikiana kikamilifu na mamlaka za Japan katika uchunguzi wa tukio hilo, huku pia ikitoa salamu za pole kwa familia ya marehemu.

Waziri wa Ulinzi wa Japan, Shinjiro Koizumi, alisema mwili wa mwanamke huyo ulipatikana mapema Jumamosi katika hoteli moja jijini Naha, mji mkuu wa Mkoa wa Okinawa.

"Tukio kama hili halikubaliki kabisa na linanikasirisha sana," Koizumi aliandika kwenye mitandao ya kijamii. "Matukio na ajali zinazohusisha vikosi vya Marekani husababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hili na hayapaswi kujirudia."

Ubalozi wa Marekani mjini Tokyo ulisema unaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ya Japan pamoja na polisi wa eneo hilo katika uchunguzi wa kesi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan ilisema ilimwita Balozi wa Marekani nchini humo, George Glass, kwa mazungumzo kuhusu tukio hilo siku ya Jumapili.

Okinawa ni makazi ya idadi kubwa ya vituo vya kijeshi vya Marekani na maelfu ya wanajeshi wa Marekani, huku matukio yanayohusisha wanajeshi hao mara kwa mara yakizua mjadala na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI