Askofu wa zamani wa Kanisa Katoliki nchini Australia, Christopher Saunders, amehukumiwa kifungo cha miaka sita na nusu jela kwa kuwanyanyasa kingono vijana wawili wa jamii ya Waaborijino wakati alipokuwa kiongozi wa kidini.
Saunders, ambaye alijiuzulu wadhifa wake wa Askofu wa Broome mwaka 2020 baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, alipatikana na hatia mwezi Agosti kwa kosa moja la ubakaji na makosa 12 ya shambulio la aibu.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 76 alihukumiwa Jumatano kifungo cha miaka sita na nusu gerezani, lakini atakuwa na haki ya kuomba kuachiliwa kwa masharti mwezi Februari 2031.
Anatajwa kuwa mmoja wa viongozi wa ngazi za juu zaidi wa Kanisa Katoliki duniani kuwahi kufikishwa mahakamani kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono.
Mahakama katika jimbo la Western Australia ilielezwa katika ushahidi kwamba Saunders aliwakaribia na kuwajengea utegemezi vijana hao kwa utaratibu, akiwakaribisha katika mikusanyiko aliyoiita ya “shirts-off”, kuwapatia pombe, na mara nyingi akitumia fedha za kanisa pamoja na mali zinazomilikiwa na kanisa kufanya hivyo.
Alipatikana na hatia ya kuwabusu na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji wa kingono vijana hao wawili. Katika tukio moja lililotokea kati ya mwaka 2010 na 2019, alihukumiwa kwa kumlazimisha mmoja wao kufanya tendo la ngono kwa njia ya mdomo.
Mashtaka kadhaa mengine ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto yaliondolewa kabla ya kesi kuanza. Pia, majaji walimkuta hana hatia katika mashtaka yaliyohusisha kijana wa tatu.
Katika taarifa ya athari kwa mwathirika iliyowasilishwa mahakamani, kijana huyo wa tatu alisema amekuwa akipata ugumu mkubwa kuzungumzia yaliyomtokea kutokana na athari za tukio hilo katika maisha yake.






0 Comments