NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka maafisa ununuzi, wanasheria na viongozi wa taasisi za umma kuhakikisha sheria na kanuni za ununuzi wa umma zinatekelezwa kikamilifu ili kulinda thamani ya fedha za umma na kuhakikisha kila shilingi ya mlipakodi inaleta matokeo yanayokusudiwa.
Dkt. Mganga ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024, pamoja na matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwanjia ya kielektroniki (NeST), mafunzo yaliyoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Amesema ulinzi wa thamani ya fedha za umma ni wajibu wa kila taasisi, akisisitiza kuwa fedha za walipa kodi zinapaswa kutumika kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani halisi ya miradi na huduma zinazotekelezwa.
“Kila shilingi ya mlipakodi inapaswa kutumika katika kuleta matokeo yanayolingana na thamani halisi ya mradi au huduma iliyopitishwa, bila kuwepo kwa uvujaji wa fedha za umma au ununuzi wa bei za juu kuliko bei ya soko,” amesema Dkt. Mganga.
Aidha, Dkt. Mganga ameeleza kuwa sheria na kanuni mpya zimeweka msisitizo katika utoaji wa fursa za ununuzi wa umma kwa makundi maalum, wakiwemo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu pamoja na wazalishaji na kampuni za ndani.
Ametoa wito kwa maafisa ununuzi na wanasheria kuhakikisha fursa hizo zilizowekwa kisheria zinatumika ipasavyo na kwa uwazi, ili kuongeza ushiriki wa makundi hayo katika shughuli za kiuchumi kupitia ununuzi wa umma.
Kuhusu mfumo wa NeST, Dkt. Mganga amesema mfumo huo unawezesha mchakato wa ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya kidijitali kuanzia hatua ya uandaaji wa mipango ya ununuzi, utoaji wa matangazo ya zabuni, upokeaji wa zabuni, tathmini, upekuzi wa mikataba hadi utekelezaji wa mikataba.
Amesema matumizi sahihi ya mfumo huo ni muhimu katika kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika mchakato wa ununuzi wa umma.
Kwa mujibu wa Dkt. Mganga, zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika kupitia taratibu za ununuzi wa umma, jambo linaloifanya sekta hiyo kuwa na nafasi muhimu katika ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema Serikali kupitia PPRA imeweka msisitizo katika utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, hususan katika maeneo ya kuimarisha utawala bora, uwazi na uadilifu, pamoja na kukuza ushiriki wa wazawa na kampuni za ndani katika fursa za ununuzi wa umma.
Hata hivyo, Dkt. Mganga amesema moja ya changamoto inayohitaji kupewa kipaumbele ni utekelezaji wa mikataba ndani ya mfumo wa NeST, ili kupunguza migogoro, ucheleweshaji wa miradi na gharama zisizo za lazima zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mikataba.
Amesisitiza umuhimu wa washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa watakayoyapata katika kuboresha utekelezaji wa taratibu za ununuzi katika taasisi zao na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Mafunzo hayo yanawaleta pamoja zaidi ya washiriki 150, wakiwemo wanasheria, maafisa ununuzi na ugavi pamoja na viongozi kutoka taasisi mbalimbali zinazotekeleza shughuli za ununuzi wa umma.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uelewa na uwezo wa watendaji hao katika matumizi ya sheria, kanuni na mfumo wa NeST, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma kwa wananch
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa magunzo hayo yatawasaidia katika utendaji kazi wao.

.jpeg)

.jpeg)





0 Comments