Na Elisante John, Matukio Daima Media.
Jumatatu, Septemba 7, 2026.
SINGIDA;Wakazi wa Manispaa ya Singida wameanza kukabiliwa na uhaba wa nyama baada ya wafanyabiashara wa nyama kugoma kuuza bidhaa hiyo, wakipinga uamuzi wa Halmashauri ya Manispaa wa kuhamisha shughuli za uchinjaji kutoka machinjio ya zamani Mitunduruni kwenda machinjio mapya yaliyopo Mtaa wa Ng’aida.
Mgomo huo umefanyika leo, Septemba 7, 2026, na kusababisha baadhi ya mabucha kufungwa, huku yale yaliyofunguliwa yakiuza nyama iliyobaki kutoka siku ya Jumapili.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, mmoja wa wafanyabiashara hao, Gwau Gwau, amesema wameamua kusitisha shughuli hizo kutokana na kutoridhishwa na miundombinu iliyopo katika machinjio mapya ya Ng’aida.
Kinyeto, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kindai, amesema miundombinu muhimu katika machinjio hayo imekamilika, ikiwemo barabara ya kuingia na kutoka, ulinzi, eneo la kuchinjia, pamoja na mifumo ya usafi na usalama.
Amesema uamuzi wa kuhamia machinjio mapya umepitishwa katika vikao mbalimbali vya Halmashauri, ikiwemo Baraza la Madiwani, hivyo wafanyabiashara hawana hiari ya kuendelea kutumia machinjio ya zamani.
“Hatuwezi kurejea kwenye machinjio ya zamani. Vikao vyote muhimu, ukiwemo mkutano wa Baraza la Halmashauri, vimepitisha machinjio mapya yaanze kufanya kazi. Sasa hapa si hiari, bali ni lazima tuende kwa maslahi ya Halmashauri yetu,” amesema Kinyeto.
Amewataka wafanyabiashara hao kuheshimu uwekezaji uliofanywa na Halmashauri, akisema hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika sekta ya mifugo na kuongeza mapato ya Manispaa kupitia kodi na ushuru unaotokana na biashara ya ng’ombe.
Naye Mwenyekiti wa zamani wa Soko Kuu la Ipembe, ambako kuna idadi kubwa ya mabucha, amepongeza hatua ya kuhamisha machinjio, akisema uamuzi huo unaweza kuleta tija zaidi kwa Manispaa na wafanyabiashara kwa siku zijazo.
MWISHO
MATUKIO DAIMA MEDIA IMETEULIWA KUWANIA TUZO ZA SKA2026 TUNAOMBA KURA YAKO WAWEZA KUPIGA KURA KIRAHISI KULIKO KUPITIA LINK HII⬇️⬇️⬇️








0 Comments