Header Ads Widget

WATUMISHI HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI WAONDOA SIKIO LA KUFA SHULE YA SEKONDARI SINDE

 



Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wamejitolea kusaidia sekta ya elimu mkoani Mbeya kwa kuchanga fedha na kununulia Shule ya Sekondari ya Sinde mashine kubwa ya kisasa ya kudurufu nyaraka (photocopy) ili kutatua changamoto ya uandaaji wa mitihani ya wanafunzi.

Msaada huo unalenga kuwaondolea adha wanafunzi wa shule hiyo ambao hapo awali mashine iliyokuwepo ilipata hitililafu na walilazimika muda mwingine kufuata huduma za kudurufu nje ya maeneo ya shule, hali iliyokuwa inachelewesha na kukwamisha ufanisi wa taaluma.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji  ameeleza kuwa watumishi wa Hospitali wameonelea ni vema kuunga mkono jitihada za serikali kwa kuwekeza nguvu kuanzia ngazi ya chini ambako wataalamu wa baadaye wanapikwa.

"Sisi kama taasisi ya afya tunapokea watu ambao wameshakuwa wataalamu kama wauguzi, madaktari na fani nyinginezo. Tulifikiri na kuona ni vyema tuchangie kule wanakonolewa na kuandaliwa, ikiwemo shule hii. Serikali inafanya kazi kubwa lakini mahitaji ni makubwa, hivyo tukaona nasi tutoe mchango wetu.," alisema Dkt. Mbwanji.

Ameongeza kuwa kuwawezesha wanafunzi hao kielimu ni kuandaa tegemeo la kesho la taifa, kwani ndiko watakakopatikana madaktari na wauguzi wa baadaye, na msaada huo utawajengea uwezo wa kusoma kwa urahisi zaidi.

Naye Mkurugenzi wa wa Utawala na Rasilimali Watu Bi.  Myriam Msalale na Afisa Rasilimali Watu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Jacqueline, pamoja, walibainisha kuwa msaada huo ni kielelezo cha imani yao kwamba kazi zitakazodurufiwa kwenye mashine hiyo yatawasaidia wanafunzi kupata ufahamu wa kutosha na hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu wa mitihani yao.

Akishukuru kwa niaba ya jumuiya ya shule, Mkuu wa Shule ya Sekondari Sinde, Bi. Anatalia Valence Luwungo, amemshukuru watumishi na Uongozi wa hospitali na kueleza kuwa shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1,196 bila kuwa na mashine ya photocopy ilikuwa ni mtihani mzito, na kwamba ujio wa vifaa hivyo vya kisasa ni ukombozi mkubwa.

Nao wawakilishi wa wanafunzi wa shule hiyo Noel Sanga na Vanesa Kyando wametoa shukrani zao wakieleza kuwa zawadi hiyo ya mashine itakuwa chachu na kichocheo kikubwa kwao kuongeza bidii katika masomo ili kupata ufaulu wa juu zaidi.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI