Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
CHAMA cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) kimekusanya Sh milioni 55 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Maarifa na ofisi za chama hicho, hatua inayolenga kuimarisha maendeleo ya taaluma ya usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka nchini.
Mwenyekiti wa TRAMPA, Devotha Mrope, amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 14 wa chama hicho uliofanyika chini ya kaulimbiu, “Kumbukumbu ni Uhai wa Taasisi na Taa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Alisema hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho kutunukiwa kiwanja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2023, ambacho kitatumika kujenga kituo hicho pamoja na ofisi za TRAMPA.
Mrope amesema kituo hicho kitakuwa sehemu muhimu ya kukuza maarifa na kuimarisha taaluma ya usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka, ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika historia ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 50.
Amesema taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa sera, uongozi na mipango ya maendeleo ya Taifa, kwa kuwa kumbukumbu na nyaraka sahihi huwezesha taasisi kuhifadhi taarifa muhimu na kuzitumia wakati wa kufanya maamuzi.
“TRAMPA imeendelea kuimarisha taaluma hii kupitia mikutano, semina na mijadala ya kitaaluma tunahamasisha pia matumizi ya taarifa na takwimu katika mipango na maamuzi ya taasisi,” amesema Mrope.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwamo baadhi ya taasisi na sekta binafsi kutotumia kikamilifu takwimu katika mipango na maamuzi pamoja na ukosefu wa bajeti ya kutosha kwa shughuli za taaluma hiyo.
Amesema Serikali inapaswa kuweka mazingira wezeshi na kutenga bajeti ya kutosha ili kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu na matumizi ya taarifa sahihi katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, alizitaka taasisi za umma kuimarisha ofisi za masjala kwa kuweka miundombinu ya TEHAMA.
Kikwete amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali katika uzalishaji, usimamizi, matumizi na utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka yataongeza tija na kasi ya utoaji wa huduma.
Amesema Serikali Mtandao imeendelea kufungua fursa katika eneo la TEHAMA, ikiwamo mfumo wa e-Filing, hivyo kuwataka wataalamu wa kumbukumbu kutumia fursa hizo kuongeza ujuzi na kuwasaidia wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo.
Aidha, Kikwete amemtaka Katibu Mkuu wa Utumishi kuhakikisha wataalamu hao wanapata fursa za kuendelea na elimu ya juu, ikiwamo mafunzo ya nje ya nchi pale inapohitajika, kwa kutenga bajeti.
Amewataka wataalamu hao kuzingatia uzalendo, uadilifu, weledi na nidhamu ya kazi, pamoja na kutunza siri za Serikali na kutumia teknolojia kwa usahihi katika kutekeleza majukumu yao.









0 Comments