Header Ads Widget

SERIKALI YAANDAA MKAKATI WA KUONGEZA UZALISHAJI WA VIFARANGA BORA VYA SAMAKI

 


 Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa vijana na wajasiriamali wanaofuga samaki ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha vifaranga bora, hatua inayolenga kupunguza uhaba wa vifaranga hivyo nchini.


Hatua hiyo imekuja kufuatia ongezeko la mahitaji ya vifaranga bora linalochangiwa na kukua kwa teknolojia za uzalishaji na ufugaji wa samaki kwa kiwango kikubwa nchini.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa vijana zaidi ya 60 kutoka mikoa mbalimbali nchini, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Janeth Rukanda, amesema lengo la Serikali ni kuwajengea uwezo vijana wengi zaidi kuhusu uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki.

Rukanda amesema hatua hiyo itawawezesha vijana kufanya ufugaji wa samaki kwa tija, kuongeza kipato chao na kuongeza idadi ya wataalamu na wajuzi katika sekta ya ufugaji wa samaki nchini.


Amesema tafiti zilizofanyika katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa vifaranga vya samaki. Hata hivyo, amesema ongezeko hilo limekwenda sambamba na kuongezeka kwa mahitaji ya vifaranga kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika sekta ya ufugaji wa samaki.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi

(FETA)  Merisia Mparazo, amewataka vijana wanaoshiriki mafunzo hayo ya siku nne kuzingatia kwa umakini mafunzo wanayopewa, akisema ujuzi watakaoupata utawasaidia kufanya ufugaji wenye tija na kujikwamua kiuchumi.


“Bila kuzingatia mafunzo haya, mtakuwa mmefika hapa bila kufahamu vizuri kuhusu ufugaji. Msipokuwa makini na kuwasikiliza ipasavyo wakufunzi, mtaondoka bila kupata maarifa ya kutosha. Hili litakuwa hasara kwenu na kwa Serikali, kwa sababu mafunzo kama haya yanatumia gharama kubwa,” alisema Mparazo.



Miongoni mwa vijana wanaoshiriki mafunzo hayo ni Gojo Muhammed na Radhia Suleiman, ambao wameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwapatia mafunzo hayo, wakisema yatawasaidia kuongeza ujuzi na kuwajengea uwezo wa kuzalisha vifaranga bora vya samaki.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI