Header Ads Widget

TANI 18 ZA DAWA ZA KULEVYA ZAKAMATWA, 289 WAKAMATWA

Na Matukio DaimaMedia

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 18,078.41 za dawa za kulevya katika opresheni zilizofanyika katika mikoa 14 nchini, huku watuhumiwa 289 wakikamatwa.

Akizungumza na waandishi wa habari wa jijini Dar es Salaam Kamishna mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya(DCEA) Aretas Lyimo amesema operesheni hizo zilizofanyika kati ya Julai na Septemba 2026 zilihusisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Aidha, katika dawa zilizokamatwa, bangi zilikuwa kilogramu 11,504.76, mirungi kilogramu 6,529.5, skanka kilogramu 44.45 na heroini gramu 41.25, huku watuhumiwa 169 wamefikishwa mahakamani, huku taratibu za kisheria zikiendelea kwa wengine.

"Operesheni hizo pia ziliwezesha kukamatwa kwa vyombo mbalimbali vilivyodaiwa kutumika katika usafirishaji wa dawa hizo, vikiwamo magari manane, bajaji moja na pikipiki 40".amesema

Kwa upande wa bangi, Morogoro iliongoza kwa kukamatwa kilogramu 6,299.24 pamoja na kilogramu 226 za mbegu za bangi, huku Tabora ikikamatwa kilogramu 4,650.86 za bangi na kilogramu 203 za mbegu zake.

Hata hivyo, amesema mirungi nayo ilibainika kusafirishwa kwa kutumia pikipiki na mabasi ya abiria, hasa katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma. Katika tukio moja, basi la RATCO lenye namba T.443 EMG lililokuwa likitoka Tanga kwenda Dar es Salaam lilikutwa na vifurushi 238 vya mirungi vyenye uzito wa kilogramu 125.33.

Sambamba na hilo amesema katika Bandari ya Dar es Salaam, ukaguzi wa abiria uliwezesha kukamatwa kwa raia wa Uturuki aliyekuwa na gramu 1.87 za skanka, raia wa Kenya aliyekuwa na gramu 3.89 za mirungi na raia wa Nigeria aliyekuwa na gramu 4.6 za bangi. Arusha, raia wawili wa Afrika Kusini walikamatwa wakiwa na jumla ya gramu 65.8 za skanka.

Hata hivyo, amesema DCEA pia imezuia kuingia nchini kwa mzigo wa asidi ya sulfuriki wenye uzito wa kilogramu milioni 64 baada ya uchambuzi wa mfumo wa kielektroniki kubaini taarifa zisizo sahihi kuhusu uagizaji wake na kutokuwepo kwa maelezo ya kutosha kuhusu matumizi yake halali.

Aidha, DCEA imewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri kuimarisha udhibiti wa mizigo, ukaguzi na usimamizi wa wafanyakazi ili kuzuia magari, mabasi na pikipiki kutumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya. Aidha, imewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uuzaji na usafirishaji wa dawa hizo pamoja na vitendo vya rushwa vinavyohusiana na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI