Header Ads Widget

MADEREVA WALIA NA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI

Na Angel Magesa (UoI), Matukio Daima Media

IRINGA: Madereva wa malori wanaofanya safari katika barabara kuu ya Iringa–Mbeya wameiomba Serikali kuangalia maslahi yao na kuwashirikisha katika uundaji wa sheria na kanuni zinazohusu sekta ya usafirishaji.

Wamesema kazi hiyo ni tegemeo lao na familia zao, lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kusimama kwa muda mrefu barabarani, mazingira magumu ya kazi na kipato kisichokidhi mahitaji.

Dereva Yunus Khamis alisema udereva unapaswa kutambuliwa kama ajira yenye maslahi na mazingira bora ya kazi.

“Sisi tunaendesha magari, lakini hizi ni fursa na ni sehemu ya maisha yetu.

 Tunaomba tujipambanue kama wafanyakazi wengine, tupate maslahi ili kazi yetu iweze kulipa,” alisema.

Naye dereva Majuto alisema madereva wanapaswa kushirikishwa katika maamuzi na sheria zinazowahusu ili changamoto zao zizingatiwe.

“Tunaomba hiyo sheria iangaliwe na ifanyiwe marekebisho. Siyo kila sheria ikitungwa sisi tukiwa nyumbani tunapaswa kuitumia kazini,” alisema.

Kwa upande wake, Jacob Ignas alisema kusimama kwa malori kwa muda mrefu huwapotezea muda wa kufanya kazi na kupata kipato.

“Wazazi wangu wanategemea, familia yangu inategemea, kwa hiyo wakati mwingine sielewi nifanye nini,” alisema.

Madereva hao wameiomba Serikali na wadau wa usafirishaji kuchukua hatua kuhusu mazingira ya kazi, maslahi yao na ushirikishwaji katika maamuzi yanayohusu sekta hiyo.

Nao abiria na watu wanaojishughulisha na shughuli za usafirishaji katika Stendi ya Mabasi Iringa wamekumbwa na changamoto baada ya kukosekana kwa mabasi ya kusafiri, hali iliyosababisha baadhi yao kukaa stendi kwa muda mrefu bila kupata usafiri wa kuelekea maeneo mbalimbali.

Akizungumza katika stendi hiyo mmoja wa watoa huduma za kukata tiketi, Mwanaidi Amiri amesema hali ya usafiri kwa siku ya leo imekuwa changamoto kutokana na mgomo uliotokea hakuna magari yaliyoingia wala kutoka.

Ameongeza kuwa hali imekuwa mbaya haswa kwa wao wanaotegemea kutoka kujitafutia ridhiki na kuacha watoto nyumbani siku yao ya leo imeisha vibaya.

Nae mmoja wa abiria Editha Elias ambae alikuwa akisubiri  usafiri, amesema amekuwa katika stendi hiyo tangu saa moja asubuhi bila kupata basi, huku akieleza kuwa maelezo wanayopewa ni kwamba kuna changamoto zinazohusiana na leseni za magari hayo na makato yanayofanyika.

"Tumekuwa hapa muda mrefu, nibtoka saa moja asubuhi, madereva tukiwauliza shida ni nini, wanasema kulingana na leseni zao kuna makato yanayokatwa kwa hiyo usafiri umekuwa changamoto sana" alisema Editha.

Kufuatia malalamiko hayo, Jeshi la Polisi Tanzania limekanusha madai yanayotolewa na dereva wa malori Iringa, limesema mfumo wa kukata pointi kwenye leseni za madereva bado haujaanza kutekelezwa, limewataka madereva kutokuwa na hofu kwa kuwa kwa sasa kinachoendelea ni uelimishaji.

Nae kamishina wa Jeshi la Polisi anayehusika na Mafunzo, CP Awadh Juma Haji amesema mpaka sasa hakuna dereva yeyote ambae leseni yake imeondolewa kwa sababu ya kukatwa pointi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI