Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Morogoro limeendelea na operesheni ya kukabiliana na wizi wa umeme na hujuma dhidi ya miundombinu yake katika Mji Mdogo wa Dumila wilayani Kilosa, huku baadhi ya wananchi wanaobainika kukiuka taratibu wakichukuliwa hatua.
Mhandisi wa Usalama na Mdhibiti wa Mapato wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Joshua Elias, amewaonya wananchi kuacha vitendo vya hujuma kwa miundombinu ya umeme pamoja na matumizi yasiyofuata taratibu, akisema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi.
Mhandisi Elias amesema wananchi wanaohitaji huduma ya umeme wanapaswa kutumia njia rasmi na kuzingatia masharti yaliyowekwa na TANESCO ili kuepuka hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao.
Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mawasiliano, Khadija Ramadhani, amewasihi wananchi wake kutokujihusisha na shughuli za kuiba umeme, badala yake kufuata sheria na taratibu za TANESCO wakati wa kupata na kutumia huduma hiyo.
Afisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Chloroquine Lung'wecha, amesema operesheni hizo ni sehemu ya juhudi za shirika kudhibiti matumizi yasiyo halali ya umeme na kulinda miundombinu yake.
Lung'wecha amewataka wananchi kushirikiana na TANESCO kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyoweza kuhujumu miundombinu na kusababisha upotevu wa mapato ya shirika.
Operesheni hiyo imekuja wakati TANESCO ikiendelea na kampeni ya kudhibiti upotevu wa mapato mkoani Morogoro, ambapo timu ya wataalamu kutoka Kanda ya Kati imewasili mkoani humo kuongeza nguvu katika utekelezaji wa kampeni hiyo.
Timu hiyo inayoongozwa na Mhandisi Nseri Mwakapalila, Boniface Ngonyani na Mhandisi Nyanda Busumbu, imefanya kikao kazi na Menejimenti ya TANESCO Mkoa wa Morogoro na kutoa mbinu za kisasa za kudhibiti upotevu wa mapato.
Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emanuali Chamoto, ameipongeza timu hiyo na kuahidi kuendeleza mikakati iliyotolewa, huku wataalamu hao wakiendelea na ukaguzi wa miundombinu ya TANESCO katika eneo la Mkundi Mawasiliano lenye miradi ya TANESCO na REA.
TANESCO imeeleza kuwa baadhi ya wateja waliobainika kukiuka taratibu za matumizi ya umeme wamesitishiwa huduma, kutozwa faini na kuchukuliwa hatua za kisheria.

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)




0 Comments