Header Ads Widget

SANGU: UCHAGUZI USIGAWANYE TALGWU


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, amesisitiza kuwa uchaguzi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) usitumike kama chanzo cha migawanyiko ndani ya chama hicho, bali uwe fursa ya kuimarisha umoja na mshikamano wa wanachama.

Sangu ameyasema hayo leo, Septemba 17, 2026, jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TALGWU, ambapo amewataka wajumbe kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani, utulivu na kwa kuzingatia Katiba ya chama.

Amesema viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kutambua kuwa uongozi ni utumishi na si kutawala, hivyo wanapaswa kusikiliza kero za wanachama na kuzitatua kwa uadilifu.

Akirejea maandiko matakatifu ya Marko na Mathayo Sangu amesema viongozi wanapaswa kuelewa kuwa nafasi ya uongozi ni ya kuwahudumia wengine na si kujiona kuwa ni wakubwa kuliko wanaowaongoza.

Sangu amewapongeza viongozi na wanachama wa TALGWU kwa kudumisha amani, utulivu na ushirikiano ndani ya chama, akieleza kuwa utulivu huo una mchango katika utulivu wa Serikali na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini haki za wafanyakazi, huku akieleza kuwa milango ya Ofisi ya Waziri Mkuu ipo wazi kupitia mfumo wa majadiliano (Social Dialogue) katika kushughulikia changamoto za watumishi.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni stahiki za uhamisho, malimbikizo ya madeni na masuala mengine yanayohusu maslahi ya watumishi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU, Tumaini Nyamhokya, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya chama hicho na Serikali, akisema mawasiliano ya karibu na viongozi wa Serikali yamesaidia kupunguza migogoro na kuleta tija kwa watumishi.

Nyamhokya amemshukuru Waziri Sangu kwa kuwa msikivu katika masuala yanayowahusu wafanyakazi, akisema ushirikiano kati ya Serikali na TALGWU ni muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi.

Amesema vikao mbalimbali vya chama, ikiwemo Kamati ya Utendaji na Baraza Kuu, vimefanyika kwa amani na utulivu, hali aliyoeleza kuwa inaonesha mazingira mazuri kuelekea uchaguzi wa viongozi.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Wandiba Ngocho, amewasilisha changamoto sita zinazowakabili watumishi wa Serikali za Mitaa, huku akiiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya wafanyakazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ngocho ametaja changamoto hizo kuwa ni ucheleweshaji wa fedha za likizo, ucheleweshaji wa malipo ya posho na leseni za huduma kwa baadhi ya watumishi wa kada za afya, stahiki za uhamisho, utekelezaji wa mfumo wa PEPMIS, miundo ya utumishi na mchakato wa kubadilishiwa kada (re-categorization), pamoja na kutofanya kazi kwa ufanisi kwa baadhi ya Mabaraza ya Wafanyakazi.

Amesema baadhi ya watumishi hupokea stahiki za likizo kwa awamu au baada ya muda uliopangwa, huku changamoto nyingine ikiwa ni kuchelewa kwa malipo ya stahiki za uhamisho kwa watumishi wanaohamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine.

Kuhusu mfumo wa PEPMIS, Ngocho amesema kuna changamoto katika utekelezaji na matumizi yake, hivyo ameiomba Serikali kuendelea kufanya maboresho yatakayorahisisha matumizi ya mfumo huo kwa watumishi.

Ameeleza pia kuwa baadhi ya watumishi hukumbana na vikwazo katika mchakato wa kubadilishiwa kada kulingana na elimu na ujuzi walioupata.

Aidha, TALGWU imeomba kuboreshwa kwa utendaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi katika halmashauri na taasisi, ili kuongeza ushirikishwaji wa wafanyakazi katika masuala yanayohusu ajira na mazingira yao ya kazi.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kutoka Kenya, Somalia na Malawi, pamoja na viongozi wastaafu wa TALGWU, akiwemo Katibu Mkuu Mstaafu, Rashid Mtega.

Akihitimisha, Sangu amewataka wajumbe kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu, huku akiwataka watakaochaguliwa na ambao hawatachaguliwa kushirikiana baada ya uchaguzi kwa ajili ya kujenga TALGWU yenye nguvu na mshikamano.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI