Na Matukio DaimaMedia
Serikali imesema Mradi wa Digital Tanzania umewezesha wananchi katika maeneo yaliyokuwa hayana mawasiliano kuanza kupata huduma za Serikali kwa njia ya kidijitali, baada ya kuwekwa minara 758 na kuboreshwa mingine 304.
Mradi huo ulioanza mwaka 2021 unatarajiwa kukamilika rasmi octoba 31, 2026, huku tathmini ikifanyika kubaini matokeo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Priscus Pancras Kiwango, Mkurugenzi wa TEHAMA, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amesema maboresho hayo yamewawezesha wananchi kupata baadhi ya huduma za Serikali kupitia simu za kawaida na simu janja.
Amesema mifumo ya taasisi mbalimbali imeunganishwa na kuboreshwa, ikiwamo ya RITA na NIDA, huku wananchi wakianza kupata taarifa za huduma za Serikali mtandaoni kabla ya kufika katika ofisi husika.
Kiwango amesema Serikali pia imeanzisha vituo 32 katika ofisi za posta za mikoa kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali katika eneo moja, ambapo vituo 27 vimeshakamilika.
Aidha, amesema watumishi 500 wa Serikali wamepatiwa mafunzo ya teknolojia zinazoibuka, huku zaidi ya vijana 50 wakipata mafunzo akili mnemba kuhusu (AI), wakipelekwa kusoma nje ya nchi katika ngazi ya uzamili , ikiwemo India, Singapore, China na Finland.
Kwa upande wake, Bakari Mwamgugu, Mratibu wa Mradi wa Digital Tanzania Project, amesema mradi huo umejikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni ikolojia ya kidijitali, muunganisho wa kidijitali na ujenzi wa uwezo.
Amesema katika eneo la ikolojia ya kidijitali, Serikali imeangalia namna sheria, sera, miongozo na taratibu zinavyoweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Mwamgugu amesema mradi pia umewezesha kuimarishwa kwa miundombinu na mifumo ya Serikali, pamoja na kuunganisha taasisi mbalimbali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mwamgugu, tathmini ya mwaka wa tano inafanyika kuangalia utekelezaji wa shughuli hizo na kubaini yaliyopangwa, yaliyotekelezwa na yale ambayo bado hayajakamilika wakati mradi ukielekea kukamilika.
Naye Paul Seaden, Mtaalamu Mwandamizi wa Masuala ya Kidijitali, amesema Benki ya Dunia imeona mafanikio makubwa katika mradi huo, hasa katika kuimarisha mawasiliano, huduma za kidijitali na ujuzi.
Amesema tathmini ya sasa inalenga kuangalia matokeo yaliyopatikana tangu mradi ulipoanza mwaka 2021, tofauti na tathmini zilizopita ambazo zilijikita zaidi katika hali ya utekelezaji kwa wakati husika.
Seaden amesema hatua inayofuata ni Serikali kuendeleza mifumo na miundombinu iliyowekwa ili iwe msingi wa maendeleo zaidi ya kidijitali nchini.







0 Comments