Na. Jacob Kasiri - Moshi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amewataka washiriki wa warsha ya kupitia Rasimu ya Mpango wa Usimamizi wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi na kutoa maoni yenye tija na yanayotekelezeka ili yaakisi vipaumbele vya uhifadhi, utalii endelevu na kuzuia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo Septemba 14, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, alisema;
“Ushiriki wa wadau ni muhimu katika kujenga mpango unaozingatia uhalisia wa Mkomazi na changamoto zinazolikabili eneo hilo, niwasihi washiriki kutumia jukwaa hili kutoa maoni yenye tija na yanayotekelezeka huku yakiakisi vipaumbele vya uhifadhi wa bioanuwai na utalii endelevu.”
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kamishna wa Uhifadhi (Mst.) Mhe. William Mwakilema akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga alisema kuwa, rasimu hiyo pia ijielekeze katika kuimarisha mahusiano kati ya hifadhi na jamii zinazoishi kando kando na hifadhi hiyo.
Aidha, Mhe. Mwakilema alisisitiza, “Mpango mzuri si ule unaobaki kwenye maandishi bali ni ule unaotekelezeka, unaopimika na unaoleta matokeo chanya kwa wananchi, shirika na Taifa kwa jumla.”
Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Massana Mwishawa alisema kuwa Rasimu ya Mpango wa Usimamizi wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi (GMP) umejikita katika programu tano ambazo ni usimamizi wa mfumo wa Ikolojia ya hifadhi na kuendeleza bidhaa na miundombinu ya utalii endelevu kwa manufaa ya hifadhi na jamii.
“Sanjari na kujenga ushirikiano na ushirikishwaji wenye manufaa kwa jamii zinazozunguka hifadhi, ulinzi wa maliasili unaozingatia matumizi ya teknolojia na uendelezaji wa hifadhi.”
Warsha hiyo ya kupitia Rasimu ya Mpango wa Usimamizi wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi (GMP) ni wa miaka kumi kuanzia 2026 hadi 2036 huku ikihudhuriwa na viongozi waandamizi wa mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, wakuu wa wilaya na Wakurugenzi kutoka wilaya za Same, Mwanga, Lushoto, Handeni, Mkinga, Korogwe na Rombo, Makamishna waandaamizi kutoka TANAPA, TAWA na TFS, wadau wa Uhifadhi na Utalii, pamoja na wawakilishi kutoka TAWIRI na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori - Mweka.




















0 Comments