Header Ads Widget

MAKAMU WA RAIS NDEJEMBI MGENI RASMI KONGAMANO LA MITAALA AFRIKA 'ACA 2026 DAR'



MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias John Ndejembi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (ACA 2026) litakalofanyika Septemba 22 hadi 25, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Akizungumza na Wanahabari September 19,2026 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba amesema tayari maandalizi yanaendelea na wageni washiriki wameanza kuwasili.

Dkt. Komba amesema kwa mara ya kwanza Tanzania itakuwa mwenyeji wa kongamano hilo kubwa la mitaala barani Afrika, baada ya kutangazwa kuwa mwenyeji wakati wa Kongamano la Tano lililofanyika Abuja, Nigeria mwaka 2025.

"Tangu kutangazwa, TET kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar tumeendelea kuratibu maandalizi ili kongamano lifanyike kwa ufanisi," amesema Dkt. Komba.

Kongamano hilo litabeba kaulimbiu isemayo "Mageuzi ya Mifumo ya Elimu Barani Afrika: Maboresho ya Mitaala, Maandalizi ya Walimu na Ubunifu Jumuishi katika Nyakati za Akili Unde na Teknolojia Zinazoibuka."

Dkt. Komba amesema kongamano ni mahususi kwa taasisi zinazobuni na kuboresha mitaala, ambapo wajumbe ni wakuza mitaala, watafiti, watunga sera, washirika wa maendeleo, walimu, wakufunzi, wahadhiri na wanafunzi wa uzamili na uzamivu kutoka Tanzania, Afrika na duniani.

Ameongeza kuwa kongamano lina umuhimu wa kimkakati kwa Tanzania kwani linaendana na Dira ya Maendeleo 2050, Ajenda 2063 ya Afrika na SDG 4, na ni fursa ya kuonesha mafanikio ya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 Toleo la 2023.

Kwa siku nne za kongamano kutawasilishwa makala 80, majadiliano, maonyesho ya bunifu na teknolojia za kielimu pamoja na ziara ya kielimu shuleni.

Matokeo yanayotarajiwa ni Azimio la Dar es Salaam kuhusu Mageuzi ya Elimu, kuidhinishwa kwa Rasimu ya Mfumo wa Afrika wa Mitaala, mapendekezo ya ujumuishaji wa AI na zana za kidijitali kwenye mitaala na kuimarisha ushirikiano wa wataalamu wa mitaala barani Afrika.

 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI