Na Fadhili Abdallah,Kigoma
TIMU ya soka ya Jom FC ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Main FM Cup kwa kuifunga timu ya Mlole Parking kwa goli moja kwa bila na hivyo kuondoka na kikombe na fedha taslim kiasi cha shilingi milioni tatu.
Mashindano hayo ambayo yalifanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kawawa Ujiji Mjini Kigoma ilishuhudiwa timu ya Mlole Parking ikishika nafasi ya pili na kupata zawadi ya fedha taslim shilingi milioni 1.5 huku timu ya Kandaga Parking kutoka wilaya ya Uvinza ikishika nafasi ya tatu na kupata zawadi ya fedha taslim shilingi milioni moja ambapo timu zote zilipata zawadi ya seti ya jezi.
Akizungumza katika mashindano hayo Katibu wa Chama cha soka mkoa Kigoma (KRFA), Omari Gindi amesema kuwa masindano hayo ni njia nzuri ya kutafuta vipaji vya wachezaji chipukizi na kuwataka waandaaji wa mashindano kama hayo kuwaalika mawakala wa wachezaji na vituo vya kukuza vipaji kuhudhuria hatua ya nusu fainali na faiinali ili kuona wachezaji wanaoweza kuwachukua.
Awali mratibu wa mashindano hayo,Pascal William ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha radio cha Main FM alisema kuwa mashindano hayo yanalenga kuwapa nafasi vijana kuonyesha vipaji vyao na kupata nafasi ya kuendelezwa ambapo msimu huu timu 16 zilishiriki na mpango wa mwakani ni kuongeza timu kufikia 16
William alisema kuwa mashindano hayo yamekuwa na mafanikio ambapo msimu uliopita wapo baadhi ya wachezaji ambao waliombwa kwenda kufanya majaribio katika timu za ligi kuu na ligi ya Championship hivyo ni wazi mashindano hayo yanayo nafasi ya kusaidia kuendeleza vipaji vya vijana hao.
Akizungumza Katika mashindano hayo Mkurugenzi wa miradi ya nishati safi wa kampuni ya Oryx gas, Jenipher Mosha alisema kuwa kampuni hiyo iligawa mitungi 60 ya gesi ya kupikia kwa timu zilizokuwa zikishiriki mashindano hayo ikiwa ni kuunga mkono mpango wa Rais Samia wa matumizi ya nishati safi.
Mwisho.






0 Comments