Header Ads Widget

KAMATI YA BUNGE YASIFU UWEKEZAJI WA TFS, YATAKA SEKTA BINAFSI KUONGEZA NGUVU KUELEKEA AFCON 2027

 


Arusha: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa juhudi za kuendeleza na kuboresha miundombinu katika maeneo ya utalii, huku ikiitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji ili kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mzava, amesema maandalizi ya mashindano hayo yanapaswa kwenda sambamba na kuboresha huduma za malazi, usafiri na miundombinu katika maeneo ya utalii, ili wageni watakaokuja nchini wapate fursa ya kutembelea vivutio na kuongeza muda wa kukaa nchini.

Rai hiyo imetolewa  Septemba 05,2026 wakati Kamati ilipotembelea Hifadhi ya Msitu wa Ziwa Duluti, Arusha, ambapo imepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TFS katika kuboresha miundombinu na kuongeza mvuto wa maeneo ya utalii.

Mhe. Mzava amesema Serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake, hivyo sekta binafsi inapaswa kutumia mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali kuongeza nguvu katika sekta hiyo.

Aidha, amewataka Watanzania kutumia fursa za utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio mbalimbali nchini, akisisitiza kuwa utalii ni fursa kwa Watanzania wote.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamadi Chande, amesema uwepo wa maeneo kama Ziwa Duluti ni fursa muhimu ya kuendeleza utalii nchini, akisisitiza kuwa maeneo hayo yanaweza kuwavutia wageni wanaokuja kwa ajili ya AFCON 2027 pamoja na Watanzania wanaotalii ndani ya nchi.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji na kuboresha miundombinu ya utalii ili kuongeza ubora wa huduma, kuvutia watalii zaidi na kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kunufaika na shughuli za utalii.











Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI