Header Ads Widget

JUHUDI ZA KUSIMAMISHA MRADI WA DANGOTE LAMU ZAGONGA MWAMBA MAHAKAMANI

Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Malindi imekataa ombi la kusimamisha mradi uliopangwa wa kiwanda cha kusafisha mafuta wa Dangote wenye thamani ya takriban Sh2 trilioni katika kaunti ya Lamu.

Uamuzi huo unafuatia kesi iliyowasilishwa na wakazi 133 wa Chandavai wanaopinga mradi huo kwa madai kwamba unatekelezwa kwenye ardhi wanayoitambua kuwa ya mababu zao.

Katika uamuzi uliotolewa Septemba 25, Jaji Jane Onyango alikataa kuidhinisha ombi hilo kama la dharura, lakini akaagiza hali ya sasa ibaki kama ilivyo hadi kesi itakaposikilizwa.

Kwa mujibu wa agizo la mahakama, hali ilivyo katika kipande cha ardhi kinachojulikana kama Land Reference No. 13061 katika eneo la Manda Magogoni, Lamu, itabaki kama ilivyo hadi Oktoba 14, wakati ombi hilo litakaposikilizwa.

Mahakama pia imeagiza walalamikiwa kupewa nyaraka za kesi na kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 14 kabla ya kusikilizwa kwa hoja za pande zote.

Wakazi hao wanadai familia zao zimekuwa zikiishi na kutumia ardhi hiyo kwa vizazi vingi na kwamba hawajapatiwa fidia ya kutosha wala mpango wa wazi wa kuwahamisha.

Kwa mujibu wa walalamikaji, sehemu za ardhi hiyo zinatumika kwa kilimo na ufugaji, huku pia zikiwa na makazi, misikiti, maeneo ya ibada za jadi na makaburi ya familia, jambo linalofanya eneo hilo kuwa muhimu kwa maisha na utambulisho wa jamii hiyo.

Mradi huo wa Dangote unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumatano mjini Lamu.

Kiwanda hicho cha kusafisha mafuta kinakadiriwa kugharimu takriban Sh2 trilioni (dola bilioni 16) na kinatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa zaidi vya aina yake barani Afrika, kikiwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku.

Mradi huo unalenga kuhudumia soko la Kenya pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI