Na CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
MADAKTARI bingwa na bingwa bobezi kutoka nchini India pamoja na taasisi mbalimbali za afya Nchini wanatarajiwa kupiga kambi wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu katika kambi maalumu itakayofanyika Jimbo la Nyamagana.
Kambi hiyo itafanyika katika Uwanja wa Nyamagana kuanzia Oktoba 9 hadi 12 mwaka huu, huku wananchi wanatarajiwa kunufaika na kambi hiyo maalumu ya matibabu itakayohusisha madaktari bingwa na bingwa bobezi kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, John Nzilanyingi, alisema kambi hiyo itawakutanisha madaktari kutoka taasisi mbalimbali za afya nchini pamoja na wataalamu kutoka India.
Nzilanyingi ameeleza kuwa miongoni mwa taasisi zitakazowakilishwa katika kambi hiyo ni Taasisi ya Saratani ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa MOI, Ocean Road, Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Hospitali ya Nyamagana na Sekou Toure.
“Madaaktari hawa watakuja maalumu kwa ajili ya kutibu wananchi magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo, hivyo nawaomba wenye changamoto za kiafya katika sehemu mbalimbali kuweza kujisajili katika maeneo yao ili tuweze kupata idadi yao,” alisema.
Nzilanyingi alisema uwepo wa wataalamu hao utatoa fursa kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za kiafya kupata uchunguzi na matibabu bila kulazimika kufuata huduma hizo katika maeneo ya mbali.
Alisema wananchi wenye changamoto za kiafya wanapaswa kutumia fursa hiyo kujisajili mapema ili kurahisisha maandalizi ya utoaji wa huduma wakati wa kambi hiyo.
Kambi hiyo inatarajiwa kuanza Oktoba 9 na kuhitimishwa Oktoba 12 mwaka huu katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Katika hatua nyingine, Kwa upande wa huduma ya maji, Nzilanyingi amesema changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Nyamagana inaendelea kushughulikiwa kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo mradi wa maji wa Butimba.
Alisema zaidi ya Sh bilioni 76 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji, huku akimshukuru Serikali kwa hatua hizo na kumuomba Waziri wa Maji, Juma Aweso kusaidia kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika.
Kuhusu miundombinu ya barabara, Mbunge huyo lisema wananchi wamekuwa wakilalamikia uharibifu wa baadhi ya barabara na kuitaka Serikali kuhakikisha ubora wa kazi katika ujenzi na matengenezo ya barabara unasimamiwa ipasavyo.
"Wananchi wengi sana wamekuwa wakilalamika kuhusu uharibifu wa miundo mbinu katika jimbo la Nyamagana" alisema.

.jpeg)
.jpeg)






0 Comments