NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
WATUMISHI wa umma Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza wametakiwa kuachana na utendaji wa mazoea na badala yake kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao.
Kauli hiyo imetolewa jana septemba 28, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamdun wakati akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Misungwi ambapo ameeleza kuwa kuna baadhi ya watumishi wamekuwa na utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea, hali inayoweza kusababisha wananchi kuzungushwa wanapofika katika ofisi za Serikali kwa ajili ya kupata huduma.
Cp Hamdun ameeleza kuwa utumishi wa umma unaongozwa na sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali, hivyo watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi hiyo badala ya kutumia mazoea katika kuwahudumia wananchi.
“Tumekuwa na mila na desturi ya kufanya kazi kwa mazoea, tunashindwa kuwahufumia wananchi ili kuweza kutatua changamoto zao, matokeo yake mnaanza kuwazungumza na kushindwa kufanya kazi kwa maadili" Alisema Hamduni.
Ameleeza kuwa watumishi wanapaswa kubadili mwenendo huo na kuhakikisha wanashughulikia kero za wananchi kwa wakati, huku wakipunguza urasimu usio na sababu ili utumishi wa umma uwe na tija na wananchi waridhike na huduma wanazopatiwa.
Aidha, amesisitiza kuwa ziara za viongozi hazipaswi kuwa mbadala wa utatuzi wa kero za wananchi, bali watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuzingatia dhamana waliyopewa.
Katika hatua nyingine Cp Hamdun amewataka wananchi wa Misungwi kuheshimu sheria na kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya Serikali, akiwemo shamba la mifugo la Serikali Mabuki ambalo, kwa mujibu wa maelezo yake, lina mipaka na hati.
Amesema uvamizi wa eneo hilo ni jambo linalokiuka sheria, huku akieleza kuwa kumekuwa na matukio ambayo nyuma yake baadhi ya viongozi wa kisiasa wamehusishwa.
Amewataka wananchi kutambua kuwa kuwa kiongozi wa chama cha siasa si ruhusa ya kujiingiza katika masuala yanayokiuka sheria, akisisitiza kuwa kiongozi yeyote anayebainika kufanya vitendo vya aina hiyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria bila kujali nafasi yake.
“Niwaombe wananchi wa Misungwi kutii sheria bila shuruti. Kuwa kiongozi wa chama haikupi uhalali wa kujiingiza katika masuala ya nchi au jinai ya namna yoyote ile. Ukibainika utashughulikiwa, awe na nafasi yako na chama tutamweka pembeni tukiamini chama hakijakutuma ukatende mambo ya ajabu,” Alisema Hamduni.
Amesema Serikali inawaheshimu viongozi wa kisiasa na vyama vya siasa, lakini viongozi wanapaswa kuwa mfano katika jamii, ikiwemo kuwa mstari wa mbele katika kuheshimu na kuhamasisha wananchi kutii sheria.
Cp Hamdun ameonya uvamizi wa shamba la Serikali, uharibifu wa mali pamoja na kuwadhuru au kuwazuru watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kusimamia eneo hilo hautavumiliwa, na yeyote atakayehusika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Yeyote atakayeingia katika shamba la Serikali kwenda kuharibu mali na kwenda kuwazuru watumishi wa umma ambao wamepewa dhamana ya kuangalia lile shamba, ajue kabisa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria hatutakuwa na huruma na mtu yeyote anayefanya vitendo kama hivyo,” alisema Hamdun.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi, amesema katika bajeti ya mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imetenga jumla ya Sh milioni 245 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 20 vya madarasa na matundu 22 ya vyoo.
Amesema pia Halmashauri imepanga kujenga shule mpya ya sekondari katika Kata ya Igokero, pamoja na kuhamasisha vijiji na kata zote kuhakikisha wananchi wanashiriki katika shughuli za ujenzi na maendeleo.
Ameeleza kuwa hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri katika kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu na kuendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika miradi ya maendeleo.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)






0 Comments