Header Ads Widget

KAMATI YA BAJETI MKOA WA IRINGA YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO MUFINDI

 


Na Matukio Daima Media, Iringa

Kamati ya Bajeti ya Sekretariati ya Mkoa wa Iringa imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na halmashauri, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za Serikali zinazolenga kuboresha na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.

Ziara hiyo iliyofanyika Septemba 8, 2026, ilihusisha miradi ya sekta za elimu, afya na miundombinu, huku kamati hiyo ikifuatilia kwa kina mwenendo wa mapato, uratibu wa rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia mwongozo wa bajeti uliotolewa kitaifa.

Akiongoza ziara hiyo, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Venance Ntiyalundula, pamoja na wajumbe wa kamati hiyo walipata nafasi ya kusikiliza mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Kamati hiyo pia ilitoa mapendekezo na ushauri kwa wasimamizi wa miradi kuhusu namna ya kuongeza ufanisi, kuhakikisha thamani ya fedha inayotumika na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoweza kuchelewesha kukamilika kwa miradi iliyopangwa.

Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa ni kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi, mwamko mdogo wa baadhi ya wananchi katika kushiriki shughuli za maendeleo pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo kwa nyakati tofauti zimekuwa zikichangia baadhi ya miradi kutotekelezwa au kutokamilika kwa muda uliopangwa.

Pamoja na changamoto hizo, kamati imebaini mafanikio katika utekelezaji wa miradi, hususan kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa walimu na wanafunzi, pamoja na kuimarika kwa mazingira ya kutolea huduma za afya kwa wananchi.

Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni pamoja na ujenzi wa bwalo katika Shule ya Sekondari Ifwagi, nyumba ya mwalimu Shule ya Sekondari Itona, ukarabati wa madarasa Shule ya Sekondari Ihanu, ujenzi wa majengo ya huduma za mama na mtoto katika vituo vya afya Mtwango na Mninga pamoja na ukarabati wa Stendi ya Igowole na ufungaji wa mizani eneo la Igowole.

Miradi mingine ni ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Nzivi, ujenzi wa madarasa Shule ya Msingi Nzivi, ukarabati wa Zahanati ya Kibada, ukarabati wa madarasa katika Shule ya Sekondari Mgalo, ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Maduma, ukarabati wa daraja pamoja na ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Itengule.

Kamati pia ilikagua miradi ya afya ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya Ihowanza pamoja na miradi mingine ya vituo vya afya, huku katika sekta ya elimu ikitembelea ujenzi wa Shule ya Msingi Idumulavanu ambayo ni kituo shikizi.


Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Sekretariati ya Mkoa wa Iringa kuhakikisha fedha na rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotarajiwa ili wananchi waweze kunufaika na huduma bora za kijamii.



MWISHO



MATUKIO DAIMA MEDIA IMETEULIWA KUWANIA TUZO ZA SKA2026 TUNAOMBA KURA YAKO WAWEZA KUPIGA KURA KIRAHISI KULIKO KUPITIA LINK HII CHINI ⬇️⬇️⬇️

BONYEZA HAPA KUPIGA KURA ZOTE NNE ZA MATUKIO DAIMA



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI