Header Ads Widget

DCC KATETY AWATAKA WATUMISHI WAPYA TFS KUISHI KAMA FAMILIA MOJA

 


DODOMA. Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), DCC Dkt. Hamza Katety, amewataka watumishi wapya kuishi kama timu na familia moja, wakitumia misingi ya uvumilivu, utulivu na subira katika kukabiliana na changamoto za utumishi wa umma.

Dkt. Katety amesema hayo leo, Jumanne, Septemba 15, 2026, wakati akifunga kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Dkt. Dos Santos Silayo, programu ya mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 328 iliyofanyika kwa siku mbili katika Chuo cha Mipango (IRDP–Miyuji Campus) jijini Dodoma.

Amesema watumishi hao wanapoanza safari yao ya kazi TFS wanapaswa kutambua kuwa wameingia katika taasisi yenye majukumu mapana na kwamba watakutana na changamoto mbalimbali, hivyo wanapaswa kuwa tayari kujifunza kutoka kwa watumishi waliowatangulia na kufanya kazi kwa ushirikiano.

“Sisi huku tunapokuja tunaishi kama timu, tunaishi kama familia moja. Kwa hiyo njooni mjifunze tunavyoishi. Mjue tunavyoishi na ninyi muishi kama tunavyoishi,” amesema Dkt. Katety.

Amesema maisha ya utumishi ni safari ndefu inayohitaji uvumilivu, utulivu na subira, akiwataka watumishi hao kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo hayo kama msingi wa kukabiliana na vipindi mbalimbali watakavyopitia katika utumishi wao.

Mbali na masuala ya kazi, Dkt. Katety amewataka watumishi hao kutowasahau wazazi na walezi wao mara wanapoanza kupata kipato, akisisitiza umuhimu wa kuwathamini watu waliowalea na kuwasaidia kufikia hatua hiyo ya maisha.

Amesema pia kuheshimu viongozi, watumishi waliowatangulia na watu wenye umri mkubwa kazini ni miongoni mwa misingi inayoweza kuwasaidia kujenga mahusiano mazuri na kufanikiwa katika safari yao ya utumishi.

Akihitimisha, Dkt. Katety amewakaribisha rasmi watumishi hao TFS na kuwatakia maisha mema ya kazi, akiwataka kutumia ipasavyo nyenzo na maarifa waliyopewa katika mafunzo hayo ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI