Header Ads Widget

CHINA YAIMARISHA VIKWAZO VYA USAFIRI KWA RAIA WAKE




Sheria mpya zinazosimamia safari za kwenda na kutoka China zimeanza kutumika, hatua ambayo wachambuzi wanasema itaimarisha zaidi udhibiti wa serikali kwa raia wake.

Raia wanaochukuliwa kuwa wame "dhuru" usalama wa taifa au maslahi ya China wakiwa nje ya nchi wanaweza pia kuzuiwa kuondoka China kwa muda wa hadi miaka mitatu baada ya kurejea, huku wale wanaokiuka kanuni za uingizaji na usafirishaji wa teknolojia wakikabiliwa na marufuku kama hiyo ya kutoweza kusafiri nje.

Mamlaka za China zinasema sheria hizo zinalenga "kulinda mamlaka na usalama wa taifa" na zinakanusha madai kuwa zinazuia safari za "raia wa kawaida".

Hata hivyo, wakosoaji wanasema sheria hizo mpya zinaweza kuongeza uwezo wa Beijing wa kushinikiza au kudhibiti shughuli za raia wake wakiwa nje ya nchi.

"Hii ni nyenzo nyingine iliyoundwa kudhibiti kile ambacho raia wa China wanafanya na kusema wakiwa nje ya nchi," Profesa Tom Kellogg, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria za Asia katika Chuo Kikuu cha Georgetown, aliliambia shirika la BBC la lugha ya Kichina.

"Katika baadhi ya matukio, ili kuwazuia watu binafsi kuikosoa serikali ya China wakiwa nje ya nchi au kuwaadhibu kwa shughuli zao za kutetea haki, mamlaka za usalama wa taifa hukataa moja kwa moja kutoa pasipoti," aliongeza Kellogg.

Kwa mujibu wa sheria hizo zinazoanza kutumika siku ya Jumanne, raia wa China wanaweza kuzuiwa kuondoka nchini iwapo watakiuka kanuni za uingizaji na usafirishaji wa teknolojia ambazo "zinaweza kuhatarisha usalama wa viwanda au teknolojia wa taifa".

Pia, jukwaa la serikali ya China linaloshughulikia "ukanushaji wa uvumi", lilitoa taarifa wiki iliyopita likisema sheria hizo mpya "hazizuii safari za raia wa kawaida, bali zinatumika kama hatua ya tahadhari dhidi ya maeneo yenye hatari kubwa na watu binafsi wenye mwenendo usio wa kawaida wa kusafiri".

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI