Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
KATIKA kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limebuni teknolojia inayotumia samadi ya wanyama kuzalisha gesi ya bio (biogas) kwa matumizi ya majumbani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki katika banda la JKT, Kanali Emmanuel Mwaigobeko, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Maonesho ya Nane Nane mkoani Morogoro.
Alisema teknolojia hiyo ni rahisi kutumia na inasaidia kupunguza gharama za kununua gesi ya kupikia. Ameeleza kuwa wafugaji wanaweza kutumia samadi ya mifugo kuzalisha gesi badala ya kuitupa.
"Hii ni gesi salama kwa matumizi ya majumbani. Haina gharama kubwa kwa sababu hutengenezwa kwa kutumia samadi ya wanyama," amesema Kanali Mwaigobeko.
Alihamasisha wananchi kutembelea banda la JKT ili kupata elimu kuhusu namna ya kutengeneza na kutumia teknolojia hiyo, ambayo inaweza kuwasaidia kuzalisha gesi kwa matumizi yao ya kila siku.
Pia amesisitiza kuwa matumizi ya gesi hiyo yanachangia utunzaji wa mazingira kwa kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Kwa upande wake, kijana wa JKT, Vicent Ndondo, alisema gesi hiyo hutengenezwa kwa kuchanganya samadi ya wanyama na maji kwa uwiano sawa.
"Samadi inayotumika ni ile iliyovunwa ndani ya wiki moja ili iwe bado mbichi. Huchakatwa katika hatua kuu tatu na hatimaye huzalisha gesi kwa matumizi mbalimbali ya majumbani,"alisema.
Mwisho..






0 Comments