Header Ads Widget

SERIKALI KUONGEZA THAMANI YA MAZAO YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media

SERIKALI imejipanga kuhakikisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanaongezewa thamani kupitia viwanda ili kuongeza kipato cha wananchi, kukuza biashara na kuimarisha mchango wa sekta hizo katika uchumi wa nchi.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis L. Londo, amesema matumizi ya maarifa, taarifa sahihi na teknolojia za kisasa ni muhimu katika kuongeza tija, kuboresha ubora wa mazao na kuyawezesha kufikia masoko ya ndani na kimataifa.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini hayauzwi yakiwa ghafi pekee, bali yanaongezewa thamani na kuchakatwa kupitia viwanda kabla ya kuingia sokoni.

Londo amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kujenga uchumi wenye tija na kuongeza thamani ya rasilimali zinazozalishwa nchini.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara kupitia TARURA, kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati pamoja na kuendelea kutoa ruzuku ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.

Amesema maboresho hayo yatawasaidia wazalishaji kufikisha mazao yao katika masoko na viwanda kwa urahisi, kuongeza tija na hatimaye kupata faida zaidi kutokana na shughuli zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa Utaratibu wa Koroba nchini, Geoffrey Kilenga, amesema Tanzania ina fursa kubwa ya masoko katika ukanda wa Afrika Mashariki, SADC pamoja na nchi za Ulaya, Asia na Marekani.

Hata hivyo, amesema kunufaika na masoko hayo kunategemea uwezo wa Tanzania kuzalisha mazao yenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa, hivyo matumizi ya sayansi na teknolojia ni muhimu katika kuthibitisha ubora wa mazao kabla hayajafikishwa sokoni.

Kilenga amesema mkutano huo umeonesha umuhimu wa kutumia teknolojia katika kudhibiti ubora wa mazao, akitolea mfano kifaa kipya cha AflaBox, kinachoweza kubaini kwa haraka uwepo wa sumukuvu (aflatoxin) kwenye nafaka bila kulazimika kupeleka sampuli maabara.

Amesema teknolojia hiyo itawarahisishia wakulima, wasindikaji na wanunuzi kutambua ubora wa mazao kabla ya kuyapeleka sokoni, hatua itakayosaidia kulinda afya za walaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Kilenga amewataka wananchi kununua mazao kutoka maeneo yanayozingatia viwango vya ubora na kuendelea kufuata ushauri wa wataalamu wa sekta ya kilimo ili kuhakikisha usalama wa chakula na afya ya jamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI