Header Ads Widget

TARI UKIRIGURU YAENDELEA KUINUA TIJA YA WAKULIMA KUPITIA MBEGU BORA NA TAFITI ZA MAZAO

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Ukiriguru Mkoani Mwanza imeendelea kuimarisha sekta ya kilimo kupitia tafiti zilizowezesha kupatikana kwa mbegu bora za pamba na mazao ya mizizi, hatua inayochangia kuongeza tija na kipato kwa wakulima.


Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongoro, Wilaya ya Ilemela, mtafiti kutoka TARI Ukiriguru, Mwanjia Hassan, amesema kituo hicho kina jukumu la kufanya tafiti za mazao ya pamba pamoja na mazao ya mizizi yakiwemo mihogo na viazi.

Amesema katika zao la pamba, TARI Ukiriguru imefanikiwa kugundua aina tano za mbegu bora, huku mbegu ya UKM 08 ikiwa miongoni mwa mbegu zinazotoa mavuno ya kutosha, zinazovumilia magonjwa na kulimwa katika Mikoa yote inayozalisha pamba nchini.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo pia imefanya tafiti zinazohusu magonjwa na wadudu wa pamba kwa kutumia mbinu husishi, na kueleza  kuwa matumizi ya muda mrefu ya viuatilifu yamesababisha baadhi ya wadudu kujenga usugu dhidi ya dawa.


Kwa upande wa mazao ya mizizi, Mwanjia amesema tangu mwaka 2005, TARI Ukiriguru imegundua takribani aina 27 za mbegu bora za mihogo zinazomwezesha mkulima kupata tija, huku mbegu za kalingisi na Taricass 4 na 6/7 zikiwa miongoni mwa zinazopendwa na wakulima.


Amesema pamoja na kugundua mbegu bora, taasisi hiyo imeimarisha mfumo rasmi wa uzalishaji wa mbegu za mihogo na viazi kwa kuanzisha Chama cha Wazalishaji wa Mbegu Kanda ya Ziwa, ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima.


Katika zao la viazi vitamu, amesema TARI imegundua takribani aina 20 za mbegu bora, ambapo zaidi ya aina 10 ni viazi lishe vyenye vitamini A vinavyosaidia kuongeza kinga ya mwili, kuimarisha uwezo wa kuona na kupunguza tatizo la utapiamlo.

Aidha amesema taasisi hiyo imeboresha takribani aina nane za mbegu za asili za wakulima na kuzisajili kupitia TOSCI, ikiwemo mbegu za Ukerewe na Polista.

Mwanjia amewataka wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo na kutumia teknolojia zinazotokana na tafiti za TARI ili kuongeza uzalishaji na tija, huku akibainisha kuwa changamoto iliyobaki ni upatikanaji wa soko.


Aidha amefafanua kuwa  taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya teknolojia za kuongeza thamani kwenye mazao yanayofanyiwa tafiti, akitolea mfano zao la pamba ambapo mkulima anaweza kuzalisha pamba na baadaye kutengeneza mafuta kutokana na zao hilo.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI