Na Matukio Daima Media
SERIKALI imesema itashirikiana na vyuo binafsi kuhakikisha masomo hayo ya sayansi yanapewa kipaumbele ili wapatikane wahandisi wengi nchini na kuondoa utegemezi wa kutegemea wataalamu wa kigeni.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, wakati akizungumza kwenye wiki ya tafiti na ubunifu ya Chuo cha St Joseph cha jijini Dar es Salaam.
Alisema chuo hicho kwa muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele kutoa wataalamu wa sayansi na alikitaka kuhakikisha kinaendelea kuchukua nafasi yake ya kuongoza mwa vyuo vinavyotoa wataalamu wengi wa fani ya sayansi hapa nchini.
Waziri Mkumbo alisema ametembelea maonesho ya kitaaluma ya wanafunzi wa chuo hicho na kubaini kuwa wanafunzi hao wamemudu kubuni vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuwa na manufaa kwa taifa.
“Nimejionea ubunifu mkubwa sana kwa wanafunzi wenu lakini kinachosikitisha ni kuwa ubunifu huo unaishia kuwa wazo tu haufikii mwisho kwa hiyo nawapa changamoto mhakikishe ubunifu wa wanafunzi wenu unaunganishwa na viwanda na kuwa halisi,” alisema
“Haitakuwa na maana kama mtakuwa mnabuni vitu lakini vinaishia kwenye vyuo vyenu lazima kuwe na utaratibu wa kuhakikisha mnatumia bunifu hizo kuzalisha, wanafunzi wakimaliza hapa wanakwenda kujiajiri au kuajiriwa sasa ili uajiriwe lazima uonyeshe kitu ambacho imeshafanya na kikaleta matokeo,” alisema
Alisema wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya sayansi kama St Joseph wanapaswa kuendelea kuwa wabunifu kwa kubuni vitu mbalimbali nafuu ambavyo vitakwenda kutatua changamoto mbalimbali za kwenye jamii.
Alisema amefurahishwa na namna wanafunzi wa chuo hicho walivyofanya ubunifu wa kutumia nishati safi ya kupikia majumbani wakati huu ambapo nishati safi ya kupikia imekuwa ajenda namba moja ya serikali.
“Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wake wanatumia nishati safi ya kupikia kwa hiyo nilipoona nanyinyi mmebuni matumizi ya nishati safi nilifurahi sana nawapongeza sana,” alisema Waziri Mkumbo.
Aidha, alimpongeza Makamu Mkuu wa chuo hicho na menejimenti ya chuo kwa kuanzisha vituo vitano vya uhamiri ambavyo vyote vinafundisha masuala ya sayansi kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Mnapojitita kwenye matumizi ya roboti na akili mnemba mnakwenda sambamba na dunia inakoelekea kwa sasa kama mnavyojua serikali inakwenda kutekeleza Dira 2050 na moja ya mambo yanayozingatiwa ni matumizi ya teknolojia kwa hiyo nyinyi mnatekeleza Dira ya Serikali,” alisema Profesa Mkumbo
Alimpongeza mwanzilishi wa chuo hicho kwa uamuzi wake wa kijasiri wa kuamua kuja kuanzisha chuo hicho hapa nchini katika wakati ambapo sekta binafsi ilikuwa haijakubalika kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa.
“Kwenye vyuo vinavyofundisha masomo ya sayansi St Joseph mnaongoza kwani ndio mlianza kufundisha masomo haya kabla ya wengine kwa hiyo nawaomba mhakikishe mnabaki kwenye nafasi yenu ya kuwaw kinara kwenye kufundisha masomo ya sayansi,” alise,ma










0 Comments