NA MATUKIO DAIMA MEDIA
IRINGA.
Mbunge wa Jimbo la Ismani, Emmanuela Mtatifikolo, amesema aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Hayati William Vangimembe Lukuvi, ataendelea kuishi katika mioyo ya wananchi kutokana na mchango wake katika maendeleo ya jimbo hilo na Taifa kwa ujumla.
Mtatifikolo amesema hayo wakati akishiriki Misa Takatifu ya kumaliza msiba wa Hayati Lukuvi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Idodi, Kata ya Idodi, mkoani Iringa. Akitoa salamu za pole katika misa hiyo, Mtatifikolo amesema kazi kubwa iliyofanywa na Hayati Lukuvi wakati wa uongozi wake imeacha alama kubwa kwa wananchi wa Ismani na Tanzania kwa ujumla.
Aidha, amewatoa hofu wananchi wa Ismani na kuwataka kuwa na imani naye, akisema amedhamiria kuendeleza ajenda na kazi zilizoachwa na mtangulizi wake, ikiwemo maendeleo ya barabara, kilimo, ufugaji, utalii pamoja na jitihada za kuanzishwa kwa Halmashauri mpya.
“Leo tumekusanyika hapa kutafakari maisha ya mzee wetu, baba yetu na ndugu yetu William Lukuvi. Katika ibada iliyotuongoza, tumefundishwa kwamba sisi wanadamu tunapofika mwisho wa safari yetu, tunakamilisha kazi yetu ya duniani na kuwaachia waliobaki kuendelea na majukumu”alisema
Mtatifikolo alisema kuwa siku ya leo siyo tu siku ya huzuni, bali pia ni siku ya kumshukuru Mungu kwa maisha ya marehemu na kwa mema yote aliyoyafanya wakati wa uhai wake,ninaamini kwamba wengi waliopata nafasi ya kuishi naye na kushuhudia kazi zake wanaweza kusema kuwa ameandika kitabu chake cha maisha kwa matendo mema.
“Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ismani, tunasema wazi kwamba William Lukuvi ataendelea kuishi katika mioyo yetu kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa wananchi,Baba huyu aliikuta Ismani ikiwa na changamoto nyingi za maendeleo, na mimi ninafahamu kwa sababu ninaishi hapa”
“Wakati huo kulikuwa na changamoto kubwa za usafiri na huduma mbalimbali za msingi, lakini kupitia uongozi wake na juhudi zake, alishiriki kwa kiasi kikubwa katika kuleta mabadiliko na kusukuma maendeleo ya jimbo hili”alisema
Alisema kuwa wanapomuaga mzee wetu William Lukuvi, tumuenzi kwa kuendeleza yale mema aliyoyaacha nyuma, tusiishie kulia na kumkumbuka kwa maneno pekee, bali tuhakikishe kazi na misingi ya maendeleo aliyoiweka vinaendelea.
Kwa wananchi wa Ismani, viongozi na familia, huu ni wakati wa kuendelea kuwa na umoja, mshikamano na upendo kama alivyokuwa akihimiza wakati wa uhai wake.
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa nafasi ya kuishi na kiongozi huyu na kushuhudia kazi zake, na tunaomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Kwa upande wake Mjane wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ismani, William Lukuvi,Germana Lukuvi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na familia wakati wa msiba wa mpendwa wao na kuhakikisha anapatiwa mazishi ya heshima ya kitaifa.
Akizungumza katika shughuli za maombolezo, mjane huyo amesema familia imetambua na kuthamini mshikamano uliooneshwa na Serikali katika kipindi kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao,amesema familia pia inamshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya Lukuvi, akimtaja kama baba, mume, mtumishi wa Serikali na kada mtiifu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amewashukuru wananchi wa Jimbo la Ismani kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwatumikia kwa kipindi cha miaka 30, akisema mchango wake katika jamii na taifa utaendelea kukumbukwa.
“Nawaomba ndugu, jamaa, viongozi na wananchi kuendelea kumuombea marehemu Lukuvi ili Mwenyezi Mungu ampokee katika ufalme wake na amsamehe makosa yake”
Pia ametoa wito kwa waombolezaji kushiriki katika ratiba mbalimbali za maombolezo na shughuli za mwisho za kumuaga mpendwa wao, huku akitoa shukrani kwa wote walioshiriki kufanikisha mazishi hayo.









0 Comments