Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MELI kongwe ya Mv Liemba ambayo imekaa bila kufanya kazi kwa miaka minane inatarajia kuanza safari Septemba Mosi mwaka huu baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Meneja mradi wa ukarabati wa meli hiyo, Mhandisi Elias John Kivara akitoa taarifa kwa Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliyetembelea meli hiyo na kushuhudia zoezi la meli hiyo kuingizwa kwenye maji na kuanza majaribio alisema kuwa kwa sasa ukarabati huo umefikia asilimia 97.
Mhandisi Kivara alisema kuwa majaribio hayo ambayo yameanza Agosti 15 yatakwenda hadi kufikia Agosti 21 mwaka huu na baada ya hapo itabaki kusubiri meli hiyo kuanza safari Septemba mosi kutoka Kigoma kuelekea bandari ya Mpulungu nchini Zambia.
Akizungumza baada ya kushuhudia meli hiyo ikianza majaribio Waziri wa uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa baada ya kukaa muda mrefu kwa meli hiyo kushindwa kufanya kazi serikali ilisikia kilio cha wananchi na kutoa fedha kiasi cha Bilioni 34 kuhakikisha meli inakarabatiwa na kuanza kazi.
Waziri Mbarawa alisema kuwa meli ya Mv.Liemba ni muhimu kwa maisha ya wananchi wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa kwani ni kichocheo muhimu kwa shughuli za biashara na uchumi kwa wananchi wa mikoa hiyo lakini kutekeleza mpango wa serikali wa kuufanya mkoa huo kuwa mkoa wa kimkakati kwa shughuli za uchumi na biashara.
Pamoja na hayo Waziri Mbarawa ametoa maagizo kwa Kampuni ya meli nchini (TASHICO) kuhakikisha meli hiyo inafanyika matengenezo muhimu kila inapotakiwa kufanyika hivyo kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa chombo hicho ili iweze kudumu kwa miaka 50.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO,Eric Hamisi alisema kuwa watazingatia taratibu zote za uendeshaji wa meli hiyo kuhakikisha inadumu kwa muda mrefu lakini kuweza kutoa huduma za uhakika kwa wananchi bila kusimamia na kwamba yale yaliytokea huko nyuma yote itakuwa historia.
Mwisho.










0 Comments