Na Matukio Daima Media,Mufindi
MENEJA wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Mufindi, Mhandisi Modest Mahururu, amepongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa Kijiji cha Kibao katika kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu ya umeme.
Amesema hatua hiyo imeanza kuleta matokeo chanya, ikiwemo kupunguza vitendo vinavyoweza kusababisha uharibifu wa miundombinu ya umeme na kusaidia kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma hiyo kwa uhakika.
Akizungumza na Matukio Daima Media, Mhandisi Mahururu amempongeza Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibao, David Luvanda, pamoja na viongozi wengine wa kijiji hicho kwa kushirikiana katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mahururu, uhamasishaji unaofanywa na viongozi hao umeleta mabadiliko ikilinganishwa na kipindi ambacho hakukuwa na kampeni za kutosha za uelimishaji kuhusu ulinzi wa miundombinu ya umeme.
Alisema upatikanaji wa umeme umeendelea kuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kila siku za wananchi, ikiwemo kuendesha mashine na shughuli mbalimbali za uzalishaji, hali inayochangia kukuza uchumi wa kaya na kijiji kwa ujumla.
“Niwaombe wananchi wawe mstari wa mbele kutoa taarifa wanapoona vitendo vinavyoweza kuhatarisha miundombinu ya umeme, hususan uchomaji moto katika maeneo ya mashamba yaliyo karibu na nguzo za umeme,” amesema.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na viongozi wa kijiji ni muhimu katika kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na moto pamoja na vitendo vingine vinavyoweza kuathiri miundombinu ya umeme.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibao, David Luvanda, amesema wananchi wamekuwa wakishirikiana na uongozi wa kijiji kutoa taarifa pale wanapoona moto au mazingira yanayoweza kusababisha madhara kwa miundombinu ya umeme.
Alisema uongozi wa kijiji umeweka utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya uchomaji moto holela, hasa wakati wa kiangazi ambapo moto unaweza kusambaa kwa kasi na kufikia maeneo yenye nguzo na nyaya za umeme.
“Sisi viongozi tumeweka siku mbili kwa wiki ambazo mtu mwenye kibali anaweza kuchoma shamba lakini ikitokea anayechoma moto hana kibali, wananchi wamekuwa wakitoa taarifa kwa viongozi ili hatua za haraka zichukuliwe kudhibiti hali hiyo,” amesema Luvanda.
Alisema utaratibu huo umesaidia kuongeza uelewa miongoni mwa wananchi na kuimarisha ushirikiano katika kulinda miundombinu ya umeme.
Katika hatua nyingine, Luvanda ameomba kupatikana kwa kumbukumbu za kihistoria zinazoonyesha lini huduma ya umeme ilianza kutolewa katika Kijiji cha Kibao, ikiwemo taarifa zinazohusiana na Shule ya Msingi Kibao.
Alisema kumbukumbu hizo ni muhimu katika kutunza historia ya kijiji hicho, ambacho kinatajwa kuwa miongoni mwa maeneo ya awali kupata huduma ya umeme.
Luvanda alisema kuwa ushirikiano kati ya wananchi, serikali ya kijiji na TANESCO ni muhimu katika kuhakikisha miundombinu inalindwa na huduma ya umeme inaendelea kupatikana kwa ufanisi.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu uharibifu au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha miundombinu ya umeme, akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu hiyo ni jukumu la pamoja kwa maendeleo ya Kijiji cha Kibao na wananchi wake.











0 Comments