Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Liberia, Jewel Howard-Taylor, ameshtakiwa kwa tuhuma za kuhusika na usafirishaji wa dawa za kulevya, utakatishaji fedha na makosa mengine kadhaa, katika uchunguzi wa kimataifa wa ulanguzi wa dawa za kulevya.
Howard-Taylor alizuiliwa hapo jana kabla ya kupanda ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts, katika mji mkuu wa Monrovia.
Mkuu wa Polisi nchini Liberia, Gregory Coleman, amemhusisha makamu huyo wa zamani na kukamatwa kwa dawa ya kulevya aina ya cocaine yenye thamani ya dola milioni 317 mwezi uliopita.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 63 bado hajatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo. Wakili wake aliiambia BBC kuwa hawezi kutoa maoni hadi Howard-Taylor afikishwe rasmi mahakamani na kusomewa mashtaka.
Howard-Taylor anakabiliwa na mashtaka yakiwemo kuingiza nchini, kuuza na kusafirisha dawa zinazodhibitiwa bila leseni, biashara haramu ya dawa za kulevya, kuchochea uhalifu na kuwezesha uhalifu.
Howard-Taylor aliingia katika siasa za Liberia baada ya aliyekuwa mume wake, Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor, kuondoka madarakani. Charles Taylor alikuwa kiongozi wa zamani wa waasi ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Liberia mwaka wa 1997 hadi 2003.
Miaka kadhaa baadaye, George Weah alimchagua Howard-Taylor kuwa mgombea mwenza wake. Alikuwa makamu wake wa rais wakati wa utawala wake kuanzia mwaka 2018 hadi 2024.






0 Comments