NA HADIJA OMARY
LINDI......Zaidi ya watoto 2,00 wenye umri wa miaka 0 hadi 8 wanaoishi mkoani Lindi waliripotiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika kipindi cha mwaka mmoja, kuanzia Julai 2025 hadi Juni 2026.
Takwimu hizo zimebainishwa katika kikao cha Kamati ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na mapitio ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, kilichofanyika mkoani Lindi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, aliwataka wajumbe kutumia majukwaa yao kuhakikisha elimu kuhusu malezi bora, ulinzi wa mtoto na haki za watoto inaendelea kutolewa kwa jamii ili kujenga mazingira yanayozingatia utu, usalama na ustawi wa watoto.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Lindi, Bahati Meshaki, alieleza kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa mtoto, afya ya akili, maendeleo ya kielimu na ustawi wake wa baadaye. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika kuzuia na kuripoti matukio ya ukatili.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Mkoa wa Lindi, Bi. Juliana Kikota, aliwakumbusha wajumbe kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo wa maisha bila kupewa chakula au kinywaji kingine, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha mtoto anakuwa na afya bora.
Baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho walieleza kuwa mjadala uliokuwa umefanyika umekuwa na tija kubwa na umeongeza uelewa kuhusu wajibu wa kila mdau katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuimarisha malezi ya watoto. Walisema wataendelea kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii katika maeneo yao.
Kikao hicho kilihusisha viongozi wa dini, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, maafisa afya kutoka halmashauri mbalimbali pamoja na wataalamu kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kulinda haki na ustawi wa watoto

.jpeg)


.jpeg)




0 Comments