KLABU ya Simba SC wameingia mashirikiano na Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kuelekea Simba Day katika kusherekea miaka 90 ya tokea kuanzishwa kwake hapa nchini, "The Pride Returns Home".
Awali wakizungumza kwenye tukio hilo maalum Jijini Arusha, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Abdul-Razaq Badru amesema:
"Leo Julai 13,2026 ni siku ya fahari kwetu Ngorongoro na Klabu ya Simba ya kuunganisha utalii na michezo kama sekta mbili ambazo zinafanya kazi pamoja kwa namna tofauti.
Tunafahamu kwamba mpira wa miguu unaunganisha watu wengi kwahiyo tunaamini kwamba tunapoamini ni fursa ya kuunganisha watu wa aina mbalimbali kupitia utalii."
"Tunapokutana leo tunafahamu kwamba katika sekta ya mpira wa miguu, Simba SC ni chapa kubwa. Tunasherekea namna chapa ambazo zitafanya kazi pamoja. Chapa mbili zitapaishana kutokana na ukubwa wake. Chapa ya Ngorongoro ni kubwa sababu ya historia, chapa hii inahusisha wanyama wa aina zote wale maarufu na kwa wingi katika eneo moja dogo."
"Sisi tunaamini wenzetu wa Klabu ya Simba wamerudi nyumbani lakini pia sababu Hifadhi ya Ngorongoro inajulikana duniani. Kutakuwa na kampeni ya Simba Visit Ngorongoro, The Pride Reurns Home na hii itakuwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 90 ya Klabu ya Simba."
"Wale wote ambao wanatembelea hifadhi na watakaokuja wajue kwamba wanachangia wafahamu kwamba wanachangia katika uhifadhi na ukuaji wa nchini yetu. Mwakani tutakuwa wenyeji wa AFCON na dunia nzima itaelekea huku hivyo tunaamini hii ni shamrashamra na tumeamua kuanza na hili. Fursa hii tuliyoipata itatupaisha zaidi."- Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Abdul-Razaq Badru.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Zubeda Sakuru amesema:
: "Tangu kuanzishwa kwa Klabu ya Simba mwaka 1936 tumekuwa tukitumia mnyama Simba. Lakini tukizungumzia hifadhi ambayo imetambuliwa hadi na UNESCO tunazungumzia Hifadhi ya Ngorongoro. Na sisi tumeona kusherekea miaka 90 kwa kurudi nyumbani ambako ni Ngorongoro. Tunaamini miaka hii 90 ya Simba ambayo tumepita mambo mengi lakini tumeweza kusimama sababu asili ya Simba ni kushinda."
"Klabu ya Simba ndio klabu inayofatiliwa zaidi Afrika Mashariki na Kati, hili sio nguvu ndogo. Hii tunaiona kama fursa pekee ya kuweza kuunganisha nguvu yetu pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Tunapokelekea katika miaka 90 tutafanya shughuli za tangu kuanzishwa kwetu katika Hifadhi ya Ngorongoro ambako tutafanya uzinduzi wa matawi na programu nyingi."
"Niwatake Wanasimba wote dunia nzima kuungana nasi katika kuadhimisha miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Simba kwa kufatilia Wiki ya Simba na shughuli ambazo tutazifanya. Lakini kwa kipekee kabisa tunapokwenda kuzindua jezi mpya lakini jezi mpya itaonekana katika Wiki ya Simba. Natoa wito wa kipekee kuungana nasi."- CEO wa Simba SC, Zubeda Sakuru.
Nae Mwenyekiti wa Bodi wa Simba SC, Crescentius Magori amesema: "Hii maana yake tumeanza count down kuelekea kwenye Simba Day. Kama kuna mkoa Simba tukija huwa tunasikia raha ni Arusha kuna wakati mwingine huwa nafatilia kwa mkuu wa mkoa kuuliza ule uwanja unaisha lini. Nadhani mkoa ambao utakuwa wa kwanza kupata shughuli ya Simba Day kwa miaka ijayo ni Arusha sababu ya ule uwanja."
"Simba ilikuwa ya kwanza kusupport utalii kwa Visit Tanzania, lakini kama mnakumbuka mwaka juzi tulizindua jezi kwa kibegi na kikaenda Mlima Kilimanjaro. Mwaka huu tumeamua kusherekea miaka 90 na kusherekea Wiki ya Simba kupitia Hifadhi ya Ngorongoro. Niwahakikishie kwa kushirikiana na Simba itakuwa na faida kwa taasisi zote mbili."
"Niwahakikishie mmefanya maamuzi sahihi kushirikiana na Simba. Simba inawafuasi kwenye mitandao zaidi ya milioni 20, kwahiyo ushirikiano huu ambao tutafanya na countdown hadi tunakwenda kuzindua tutapata wateja wengi sana wa ndani na nje. Tutumie wakati huu kutangaza product nyingi kwelikweli. Sisi tunakuhakikishia tutakusupport, tupo tayari kusupport hifadhi, utalii na uchumi wa nchi hii uzidi kupaa."- Mwenyekiti wa Bodi, Crescentius Magori.
Kwa upande wa Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, Dkt. Harrieth Mtae nae amebainisha kuwa:
"Nishukuru Klabu ya Simba kwa kukubali kuwa mshirika wetu hasa katika safari hii muhimu ya kuitangaza Tanzania kupitia michezo mbalimbali pamoja na utalii.
Leo ni mwanzo mpya ya jinsi ya sekta ya umma na taasisi za michezo zinavyoweza kushirikiana katika kuleta thamani kwa taifa letu. Tunaziunganisha chapa mbili kubwa za Afrika katika kuitangaza Tanzania."
"Bodi ya Wakurugenzi inaunga kikamilifu kwakuwa unaendana na kabisa na maono ya kuifanya Ngorongoro kuwa destination ya kiwango cha kimataifa lakini pia ikitoa mchango wa utekelezaji wa vipaumbele vya taifa vya kukuza utalii, kukuza uchumi na diplomasia ya kimkakati."
"Tunaamini kupitia kampeni ya Simba na Ngorongoro ya The Pride Returns Home, mamilioni ya Watanzania na mashabiki wa mpira wa miguu watapata sababu mpya ya kutembelea Ngorongoro na kujivunia urithi wa nchi yao.
Tunapoelekea kwenye AFCON 2027 ushirikiano huu unaonyesha kwamba michezo inaweza kuwa chombo cha kutangaza utalii, kuhamasisha uhifadhi na kuijenga Tanzania kama destination bora ya Afrika.
Kwa mara nyingine nawashukuru viongozi wa Simba Sports Club kwa maono haya ya pamoja. Tunatarajia ushirikiano wa muda mrefu utakaoleta manufaa kwa taasisi zote mbili na kwa taifa kwa ujumla. Karibuni Nyumbani, Karibuni Ngorongoro."- Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, Dkt. Harrieth Mtae.
















0 Comments